MOSHI-KILIMANJARO.
WANANCHI wametakiwa kuendelea kujisajili na kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio za Mwanga Marathon and Festival zinazotarajiwa kufanyika Desemba 20 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, kuimarisha afya zao na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo wilayani Mwanga.
Mwito huo umetolewa na Mwandaaji wa mbio hizo, Frida Mberesero, ambaye amewahimiza wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini kujitokeza kushiriki, akieleza kuwa mbio hizo ni fursa ya kuunganisha michezo, afya na utalii.
![]() |
Mberesero, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mwanga Marathon na Mkurugenzi wa kampuni ya Kisangara Tours, amesema ushiriki mkubwa wa wananchi utasaidia kufanikisha malengo ya mbio hizo, ikiwemo kuunga mkono juhudi za Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Hassan Bomboko, katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo.
Amesema Mwanga Marathon si tukio la kimichezo pekee, bali pia ni jukwaa muhimu la kuitangaza wilaya hiyo, kuvutia wageni na kutoa fursa kwa wananchi kunufaika na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazoweza kuchochewa na utalii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi na kujisajili mapema ili kupata nafasi ya kushiriki katika mbio hizo zinazolenga kuhamasisha utamaduni wa kufanya mazoezi na kukuza utalii wa ndani.
![]() |







