KAMATI YA MAADILI YAMTIA HATIANI DIWANI WA KATA YA MJIMPYA ABUU MOHAMED SHAYO KWA KUVUNJA MAADILI, ADHABU YAWEKWA WAZI

MOSHI-KILIMANJARO.

KAMATI ya Maadili ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imemtia hatiani Diwani wa Kata ya Mjimpya, Abuu Mohamed Shayo, kwa kukiuka maadili ya uongozi ikiwamo kuwadharau na kuwadhilisha baadhi ya watumishi wa umma.

Hayo yamesemwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, wakati akizungumza katika kikao cha robo ya pili ya Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo.

Amesema shauri hilo liliwasilishwa mbele ya Kamati ya Maadili baada ya diwani huyo kutuhumiwa kutumia lugha zisizofaa dhidi ya watumishi na kuingilia utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema Kamati ya Maadili imependekeza taarifa ya maamuzi yaliyofikiwa dhidi ya diwani huyo iwe sehemu ya ripoti ya uwajibikaji ya Halmashauri na kuwekwa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ili wananchi waweze kuifahamu.

Aidha amesema Kamati ya Maadili imeshughulikia mashauri ya kinidhamu ya watumishi saba wa Manispaa, ambapo watumishi wanne wamefukuzwa kazi baada ya kubainika kuwa watoro kazini kwa kipindi cha miezi 12. 

Amesema watumishi wawili wamepewa adhabu ya kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao kwa miaka mitatu, huku mtumishi mmoja akirejeshwa kazini baada ya kutokutwa na hatia, lakini ataendelea kuwa chini ya uangalizi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwaijuma Nasombe, amewataka madiwani kuwaheshimu watendaji waliopo katika kata zao na kuwaona kama watumishi wanaotekeleza majukumu kwa niaba ya Halmashauri na wananchi.

Amesema baadhi ya vitendo vinavyofanywa dhidi ya watendaji vinaweza kuwafanya washindwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na hivyo kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akitoa salamu za Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amewataka madiwani kuimarisha mahusiano na watendaji na kuheshimu mipaka ya majukumu yao.

Amesema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya madiwani na watendaji, akisisitiza kuwa changamoto zinazowahusu watendaji zinapaswa kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa, Meya au Mkuu wa Watumishi wa Wilaya (DAS), badala ya kuchukuliwa hatua binafsi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai, amewataka madiwani kujenga mahusiano mazuri na watendaji wao, kutumia lugha yenye heshima na kushirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.