SERIKALI YASITISHA UCHIMBAJI WA MORAMU, UCHONGAJI WA TOFALI MOSHI

MOSHI-KILIMANJARO.

SERIKALI ya Wilaya ya Moshi imesimamisha kwa muda shughuli za uchimbaji wa moramu na uchongaji wa tofali za miamba katika maeneo ya migodi, hatua inayolenga kuzuia uwezekano wa kutokea kwa maafa kutokana na mashimo na maeneo hatarishi wakati wa mvua zinazotarajiwa kunyesha.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, iliyoongozwa na Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Ramadhani Mahanyu, iliyokuwa ikikagua utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali, ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Alisema katika maeneo ya migodi ya Uchira, Pumuwani na Nganjoni, wananchi wamekuwa wakifanya shughuli za kuchimba moramu na kuchoronga tofali za miamba, hali ambayo imeacha mashimo mengi ambayo yanaweza kuwa hatari wakati wa mvua, hivyo Serikali imeamua kusimamisha shughuli hizo kwa muda.

“Kuna wananchi wanaofanya shughuli za kuchoronga tofali na kuchimba moramu, kumekuwa na mashimo mengi sana. Tunazisimamisha shughuli hizi katika kipindi hiki cha mvua ili kuepuka udongo ambao unaweza kuwafunika wakiwa wanaendelea na shughuli hizo,” alisema Mnzava.

Mnzava alisema hatua hiyo ni sehemu ya tahadhari zinazochukuliwa na Serikali kuelekea kipindi cha mvua zinazotarajiwa kunyesha, akieleza kuwa mashimo na maeneo yaliyofanyiwa uchimbaji yanaweza kujaa maji au udongo kumeguka na kusababisha madhara kwa wananchi wanaofanya shughuli hizo pamoja na wakazi wanaoishi maeneo ya jirani.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, John Minja, alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakichimba moramu na kutengeneza tofali katika maeneo ya migodi, hivyo ameiomba Serikali kuhakikisha shughuli hizo zinasimamishwa wakati wa kipindi cha mvua ili kuzuia uwezekano wa kutokea kwa maafa.

Minja alipendekeza migodi hiyo kufungwa kwa muda hadi mvua zitakapopungua, ndipo wananchi waruhusiwe kurejea katika shughuli za uchimbaji, huku akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na mashimo yaliyoachwa wazi.

Aidha, alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakiuza sehemu za mashamba yao kwa ajili ya uchimbaji wa mawe, ambapo baada ya wachimbaji kumaliza kuchukua mawe huacha mashimo makubwa bila kuyafukia. Amesema hali hiyo ni hatari kwa watoto na watu wazima, hasa wakati wa mvua ambapo mashimo hayo hujaa maji na kusababisha uharibifu wa mazingira pamoja na kuhatarisha usalama wa wananchi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.