MOSHI-KILIMANJARO.
KATIKA wakati ambao saratani ya matiti na shingo ya kizazi imeendelea kuwasababishia wanawake wengi maumivu na vifo vya mapema, sasa matumaini mapya yanaanza kuonekana kwa wanawake wa Moshi Mjini baada ya kutangazwa kwa huduma maalum za bure za upimaji wa magonjwa hayo.
Hatua hiyo inalenga kuokoa maisha kupitia uchunguzi wa mapema na elimu ya afya kwa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, alisema kuwa kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Jumuiya hiyo imejipanga kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, hususan wanawake, ili kuongeza uelewa na kuwahamasisha kujitokeza kupima afya zao mapema.
Alisema kuwa Umoja wa Wanawake wa Tanzania wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Moshi Mjini itafanya zoezi hilo katika Kituo cha Afya Pasua kilichopo Kata ya Bomambuzi, ambapo huduma ya upimaji wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi itatolewa bure kwa wananchi wote watakaojitokeza.
Komba alisema , mbali na upimaji wa saratani, wananchi watapatiwa elimu kuhusu magonjwa ya saratani, dalili zake na namna ya kujikinga, kutakuwa na elimu ya lishe bora, upimaji wa shinikizo la damu (pressure), kipimo cha sukari, pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu afya kwa ujumla.
Aidha, alisema kutakuwa pia na utoaji wa elimu ya Bima ya Afya kwa Wote, ambayo itatolewa ili kuwahamasisha wananchi kujiunga na mifumo ya kinga ya afya.
Komba alibainisha kuwa huduma hizo zitatolewa na wataalamu wa afya wakiwemo madaktari, huku daktari bingwa wa magonjwa ya saratani akitarajiwa kuwepo kwa ajili ya kutoa uchunguzi na ushauri wa kitaalamu kwa watakaohitaji huduma hiyo.
"Zoezi hilo linatarajiwa kuanza Machi 2 hadi tMachi 4 mwaka huu kuanzia saa 3:00 asubuhi kila siku katika Kituo cha Afya Pasua, wanawake na wananchi kwa ujumla wamehimizwa kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizo muhimu zitakazosaidia kugundua magonjwa mapema na kuokoa maisha,"alisema Komba.
Komba alitoa wito kwa jamii kuhamasishana na kuwajulisha wengine, hususan wanawake, kujitokeza kwa wingi katika siku hizo, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa vitendo na kuonesha umuhimu wa kulinda afya ya mwanamke na jamii kwa ujumla.






