NGUJINI-MWANGA.
WANANCHI wa Kata ya Ngujini, Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, wamemueleza Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mwaga Ngwaru, changamoto kubwa zinazoikabili Shule ya Msingi Changalavo, ikiwemo ukosefu wa vyoo bora na maji safi na salama.
Malalamiko hayo yalitolewa wakati mbunge huyo akiwa katika ziara ya kusikiliza na kupokea kero za wananchi katika kata mbalimbali za jimbo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Peter Mlacha, mkazi wa Ngujini, alisema shule hiyo imekumbwa na tatizo la vyoo kwa miaka mingi, huku choo kilichopo kikiwa chakavu na kisichofaa kutumiwa na wanafunzi.
“Wanafunzi wanaingia chooni katika mazingira hatarishi, miundombinu ni mibovu na hali si salama kiafya,” alisema Mlacha.
Aliongeza kuwa kutokana na changamoto hiyo, jamii iliamua kujichangisha fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa choo kipya, ambapo serikali ilitoa msaada wa shilingi milioni mbili, hata hivyo, ujenzi huo bado haujakamilika.
Kwa mujibu wa wananchi, walisema kutokana na changamoto hizo wanafunzi kutokupata chakula cha mchana shuleni kutokana na ukosefu wa maji safi na salama, pamoja na vyoo,, hali hiyo imesababisha baadhi ya wazazi kukata tamaa na kuwahamishia watoto wao katika shule nyingine.
“Wazazi wameacha kuchangia chakula kwa sababu wanauliza, watoto watakapokula na kutaka kwenda chooni, watajisafishia wapi wakati hakuna maji?” alisema Mlacha.
Maria Ambros Mruma alisema walimu na wanafunzi wanalazimika kutafuta maji mtoni kwa kubeba ndoo, hali ambayo ni hatari kiafya kwa kuwa maji hayo si salama.
“Wanafunzi wanashindwa hata kula chakula cha mchana kwa kuhofia magonjwa yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama,” alisema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwangara, Luka Nathaniel Msuya, alisema shule hiyo haina kabisa maji ya kujisafishia baada ya kutumia choo, jambo linaloongeza hatari ya mlipuko wa magonjwa hasa kipindi cha mvua.
Alima kuwa choo kilichopo ni cha zamani, kina matundu mawili tu na hakina milango, wanafunzi huingia bila kuwepo kwa mlango na kujisaidia choo kikiwa wazi.
“Ni aibu kubwa kuona watoto wanapanga foleni kusubiri kuingia chooni katika Tanzania ya leo tunayoizungumza kuwa ya maendeleo, ni vigumu hata kumleta kiongozi atembelee shule hii na kushuhudia hali hiyo,” alisema.
Kwa upande wake, Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Andrew Sangalala, alisema kiafya ni hatari kwa shule kukosa maji, na kusisitiza umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka kuzuia milipuko ya magonjwa.
Naye Afisa Elimu Msingi, Robert Tarimo, alikiri kuwepo kwa changamoto ya vyoo katika shule hiyo, akisema mfuko wa jimbo ulitoa shilingi milioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa choo, lakini haujakamilika.
Alisema katika bajeti ya mwaka 2025/2026, halmashauri imetenga shilingi milioni nne kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
“Tunasubiri fedha hizo zitoke ili ziweze kumalizia ujenzi wa choo hicho,” alisema Tarimo.
Akizungumzia changamoto ya maji, Tarimo alisema mabomba ya maji ya shule yalichomwa moto na kuharibika, hali iliyosababisha kukosekana kwa huduma hiyo.
Alibainisha kuwa mkakati uliopo ni Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuleta mabomba mapya ili kurejesha miundombinu ya maji shuleni hapo.
Diwani wa Kata ya Ngujini, Roggers Msangi, alisema hali ya vyoo katika shule hiyo si nzuri, licha ya jitihada za wananchi kuchimba shimo, kujenga msingi na kupandisha kuta.
“Changamoto imekuwa ni nguvu kazi na fedha za kumalizia ujenzi. Nimewasiliana na Mkurugenzi pamoja na Afisa Elimu kuhusu suala hili, lakini hadi sasa fedha hazijaletwa,” alisema.
Wananchi wameiomba serikali kuharakisha utoaji wa fedha zilizotengwa ili kukamilisha ujenzi wa vyoo na kurejesha huduma ya maji, kwa lengo la kulinda afya na ustawi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Changalavo







