WAZIRI WA AFYA MOHAMED MCHENGERWA; AMPONGEZA MBUNGE MOSHI MJINI KWA KUTEKELEZA AHADI ZAKE BINAFSI KWA WANANCHI


MOSHI-KILIMANJARO.

WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi zake binafsi alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akisema hatua hiyo ni mfano wa uongozi unaojali wananchi na unaojenga imani kwa wapiga kura.

Mchengerwa alitoa pongezi hizo mjini Moshi wakati wa hafla ya kukabidhi magari yatakayotumika katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi binafsi za Mbunge huyo kwa wananchi wa jimbo lake.

"Nimpongeze Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa kutekeleza ahadi zake kwa wakati, hii ni ishara ya uongozi wa kuwajibika, wabunge wengi hutoa ahadi nyingi wakati wa kampeni, lakini utekelezaji wake huwa wa kusuasua au hausikiki kabisa hadi uchaguzi unapokaribia tena," alisema Mchengerwa.

Alisema tabia ya viongozi kushindwa kutekeleza ahadi zao ndiyo sababu kubwa inayochangia kubadilika kwa sura ya Bunge kila baada ya uchaguzi mkuu.

"Kila baada ya miaka mitano kati ya asilimia 65 hadi 75 ya wabunge wanaoingia Bungeni huwa ni wapya. Mwaka 2015 wabunge wapya walikuwa asilimia 87, mwaka 2020 walikuwa asilimia 70, na mwaka 2025 wamefikia asilimia 68, jambo ambalo linaonesha wananchi wanawawajibisha viongozi wanaoshindwa kutimiza ahadi zao," alisisitiza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, alimshukuru Waziri Mchengerwa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo na kushuhudia utekelezaji wa ahadi alizowaahidi wananchi.

Shayo alisema wakati wa kampeni aliwaeleza wananchi kuwa mbali na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), angekuwa na ahadi zake binafsi ambazo angezisimamia kwa fedha na uwezo wake mwenyewe.

"Moja ya ahadi nilizotoa ilikuwa ni kuwa karibu na wananchi wakati wote, pia niliwaahidi kuwa nitatoa magari mawili aina ya Costa yatakayosaidia shughuli za kijamii, hususan katika nyakati za furaha na matatizo, leo ahadi hiyo imetekelezwa rasmi," alisema.

Aidha alisema kuwa aliahidi pia kununua gari maalumu la kubeba wagonjwa (Amblece) pamoja na gari la kubebea miili ili kusaidia wananchi wanaokumbwa na changamoto mbalimbali za kijamii, na kwamba ahadi hizo zote sasa zimekamilika.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema magari hayo ni sehemu ya ahadi binafsi ambazo Mbunge Shayo alizitoa wakati wa kampeni na kwamba utekelezaji wake unaonesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia wananchi.

"Ninatoa pongezi kwa Mbunge wetu kwa kutimiza alichowaahidi wananchi, hii ni hatua inayostahili kuigwa na viongozi wengine kwa sababu wananchi wanathamini matendo kuliko maneno," alisema Mnzava.

Naye Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, alisema ahadi hizo zilinadiwa sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kampeni za mwaka 2025, lakini zilikuwa ni ahadi zake binafsi za Mbunge ambazo hazikuwamo ndani ya ilani ya chama.

"Haya ni mambo ambayo Mbunge wetu aliamua kuyafanya kwa hiari yake ili kuongeza huduma kwa wananchi, leo tunashuhudia utekelezaji wake kwa vitendo, jambo linaloonesha uadilifu na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi waliowachagua," alisema Kidumo.

Kwa niaba ya madiwani wa Manispaa ya Moshi, Kidumo aliwataka viongozi wote waliochaguliwa kuendelea kusimamia kwa vitendo ahadi walizozitoa kwa wananchi katika kata zao.

"Na sisi madiwani tunapaswa kujifunza kutoka kwa mfano huu,turejee kwa wananchi wetu tukaendelee kutekeleza ahadi tulizozitoa wakati wa kampeni. Wananchi wanatupima kwa matokeo ya kazi zetu, si kwa ukubwa wa ahadi zetu, tukitimiza tulichoahidi, tutajenga imani, mshikamano na maendeleo ya kweli katika maeneo yetu," alisema.

Akizungumza mmoja wa wananchi walioshuhudia hafla ya makabidhiano rasmi ya magari hayo, Robert Maliviche, alisema kuwa yatasaidia kurahisisha huduma za kijamii, ikiwemo usafiri wakati wa misiba, matibabu na shughuli nyingine za kijamii ndani ya Jimbo la Moshi Mjini.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.