MOSHI-KILIMANJARO.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, ameiomba Serikali kupitia Mfuko wa Wajibu wa Mashirika kwa Jamii (CSR), kurejesha asilimia 15 ya mapato na tozo zinazokusanywa na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.
Makoi alitoa ombi hilo wakati wa kikao cha Kamati ya Siasa ya CCM Wilayani humo, kilichoketi kwa ajili ya kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava.
Alisema fedha hizo za CSR zinazotokana na shughuli za KINAPA zinapaswa kuelekezwa katika miradi ya maendeleo ya wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro, hatua ambayo alisema itasaidia kupunguza migogoro na kujenga uhusiano mzuri kati ya jamii na hifadhi.
“Tunaiomba Serikali itufikirie sisi wananchi ambao tunaishi na kutunza Mlima Kilimanjaro, tuna vijiji 40 vinavyozunguka mlima huo, kuanzia Wilaya za Hai, Moshi, Vunjo hadi Rombo,” alisema Makoi.
Alisema ili wananchi waone kuwa uwepo wa Mlima Kilimanjaro na hifadhi yake ni fursa na si hasara kwao, ni muhimu asilimia 15 ya mapato yanayotokana na tozo za utalii katika mlima huo irejeshwe kwa jamii kupitia CSR.
Makoi alisema fedha hizo zinaweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo, ikiwemo elimu, barabara, maji na miundombinu ya umwagiliaji.
Alisema hapo awali KINAPA ilikuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kusaidia jamii inayozunguka hifadhi hiyo, lakini kwa sasa hali imebadilika na hakuna kiwango cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi kwa kiwango kinachotarajiwa.
Kwa mujibu wa Makoi, katika mwaka wa fedha 2025/2026, KINAPA ilikusanya Sh bilioni 945 kutokana na mapato ya tozo za utalii, huku kiasi kilichotengwa kwa ajili ya kusaidia changamoto za jamii kinachodaiwa kuwa Sh milioni 148.
“Niliwauliza wametenga kiasi gani kwa ajili ya kusaidia changamoto ndogo ndogo katika vijiji vinavyozunguka mlima huo. Majibu waliyonipatia ni kiasi cha Sh milioni 148,” alisema.
Alisema Jimbo la Moshi Vijijini linakabiliwa na changamoto mbalimbali za maendeleo, ikiwemo uchakavu wa shule za msingi, ubovu wa barabara na ukosefu wa vyoo bora katika baadhi ya shule za msingi na sekondari.
“Tukiweza kupatiwa fedha hizi za CSR, zinaweza kusaidia kutatua changamoto hizo, kwa sababu mahitaji ni makubwa na uwezo wa bajeti za kawaida hautoshi,” alisema.
Makoi pia alisema barabara nyingi zinazozunguka vijiji vinavyopakana na Mlima Kilimanjaro hazipitiki vizuri, huku akieleza kuwa bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) haitoshi kukarabati barabara zote zinazohitaji matengenezo.
Alisema endapo sehemu ya mapato ya KINAPA ingetengwa kupitia CSR, fedha hizo zingeweza kusaidia kuboresha miundombinu hiyo na kurahisisha usafirishaji wa wananchi na mazao yao.
Aidha, Makoi alisema Wilaya za Moshi na Vunjo zina mifereji ya asili ya umwagiliaji 391, ambayo kwa miaka ya nyuma ilichangia kwa kiasi kikubwa shughuli za kilimo, hususan uzalishaji wa kahawa na ndizi.
Alisema mwaka uliopita Serikali ilitenga Sh bilioni 15.2 kwa ajili ya ukarabati wa mifereji hiyo, akisisitiza kuwa iwapo KINAPA ingetenga fedha kwa ajili hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu, zingeweza kusaidia kujenga na kukarabati mifereji hiyo na kuwawezesha wananchi kunufaika zaidi na kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, aliuomba uongozi wa KINAPA kuhakikisha jamii inayozunguka hifadhi inanufaika na miradi mbalimbali ya kijamii, pamoja na kupewa elimu ya uhifadhi ili wananchi wawe sehemu ya juhudi za kulinda Mlima Kilimanjaro.



