BUNGENI-DODOMA.
WANANCHI wa Kata ya Kirua Vunjo Mashariki, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, wanatarajia kunufaika na huduma bora za afya, baada ya wadau wa maendeleo wanaounda umoja wa LEKIDEA kuchangisha zaidi ya Sh milioni 30 zilizowezesha kununuliwa eneo la hekari sita kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha kata hiyo.
Hatua hiyo inatajwa itakwenda kuondoa changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa eneo la kujenga kituo hicho, hali iliyokuwa ikikwamisha jitihada za wananchi kupata huduma za afya karibu na makazi yao.
Akizungumza katika vikao vya maendeleo vilivyofanyika jijini Dodoma, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, alisema wadau hao wameonyesha uzalendo mkubwa kwa kushiriki moja kwa moja katika kutatua changamoto za maendeleo zinazowakabili wananchi wa Kirua Vunjo Mashariki.
Alisema baada ya kukamilisha upatikanaji wa eneo hilo, hatua inayofuata ni kuharakisha maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho ili wananchi waanze kunufaika na huduma muhimu za afya kwa wakati.
Katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Jafari Sefu, aliwapongeza wadau wa LEKIDEA kwa moyo wao wa kujitolea na kuahidi kuwa Serikali itashirikiana nao kuhakikisha maandalizi ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kirua Vunjo Mashariki yanaanza haraka iwezekanavyo.
Mbali na suala la afya, wadau hao waliwasilisha ajenda ya maendeleo ya Barabara ya Uchira–Kisomachi–Kolarie yenye urefu wa kilomita 10.8, wakikumbusha Serikali kuhusu mchango wao wa zaidi ya Sh milioni 130 pamoja na vifaa vya ujenzi wa lami vilivyowezesha kujengwa kwa kilomita 1.2 za barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Wadau hao waliiomba Serikali kutekeleza sehemu iliyobaki ya makubaliano ya kukamilisha ujenzi wa barabara yote, wakieleza kuwa mradi huo utarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Aidha, LEKIDEA iliwasilisha ombi la ujenzi wa Bwawa la Urenga, mradi unaotarajiwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa Kirua Vunjo Mashariki na maeneo jirani.
"Kukamilika kwa bwawa hilo litasaidia kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea ufugaji wa samaki."walisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Raymond Mndolwa, alipokea maombi ya mradi huo na kuagiza wataalamu wake kuanza mara moja tathmini ya mahitaji ya bwawa hilo ili hatua za awali za utekelezaji zianze kwa wakati.
Koola aliwashukuru wadau wa LEKIDEA kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya kata hiyo na kutoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo ndani ya Jimbo la Vunjo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi.









