MORRIS MAKOI; ALETA MITAMBO MIPYA KUBORESHA BARABARA KOROFI MOSHI VIJIJINI

MOSHI-KILIMANJARO.

MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Morris Makoi, amesema tayari ameanza jitihada za kukabiliana na changamoto ya ubovu wa barabara kwa kununua mitambo ya ujenzi, ambapo baadhi yake imekwishafika na mingine inaendelea kufungwa tayari kwa kuanza kazi.

Hayo aliyasema jana Aprili 8,2026, wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Uru Mashariki, wakati wa ugawaji wa miche bora ya kahawa 15,000, iliyotolewa na Bodi ya Kahawa Tanzania TCB. 

Makoi, alisema hatua hiyo inalenga kuboresha miundombinu ya barabara zote korofi katika jimbo hilo, zikiwemo zile zinazowakwamisha wananchi katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, wananchi wa Kata ya Uru Mashariki, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia ubovu wa barabara ya Rau–Mamboleo–Materuni yenye urefu wa kilometa 10.2, wakidai kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha changamoto kubwa ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa, hususan wakati wa mvua za masika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi akiwemo Patrick Ngowi na Philemon Njau, walisema barabara hiyo imekuwa katika hali mbaya kwa muda mrefu, huku ahadi za kuitengeneza zikitolewa mara kwa mara bila utekelezaji wake.

Walisema hali hiyo imekuwa ikiwasababishia usumbufu mkubwa pamoja na kuongeza gharama za usafiri, hali inayowaathiri kiuchumi na kijamii.

Naye mkazi wa eneo hilo, Samwel Materu, aliikumbusha serikali kutimiza ahadi yake ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, akieleza kuwa ahadi hiyo ilitolewa wakati wa kampeni.

Alisema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa si tu kwa wakazi wa eneo hilo bali pia kwa uchumi wa taifa, kutokana na watalii wengi kuitumia kufika katika maporomoko ya maji ya Materuni.

Diwani wa Kata ya Uru Mashariki, Onesmo Chuwa, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuziomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuitengeneza ili kuboresha huduma za usafiri.

Akifafanua zaidi, Mbunge Makoi alisema kata zinazokabiliwa na changamoto kubwa ya barabara zisizopitika ni pamoja na Uru Kusini, Mbokomu, Uru Kaskazini, Old Moshi na Kimochi, na kwamba juhudi zinaendelea kuhakikisha miundombinu hiyo inaboreshwa.


Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhani Mahanyu, alisema barabara hiyo ni miongoni mwa ahadi zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni, akiwataka wananchi kuwa na subira wakati serikali ikiendelea na mipango ya utekelezaji.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.