SERIKALI YATAJA SABABU ZINAZOCHANGIA TIJA NDOGO YA KAHAWA

MOSHI-KILIMANJARO.

WIZARA ya Kilimo imetaja sababu tano kuu zinazochangia kushuka kwa tija ya zao la kahawa nchini, zikiwemo matumizi madogo ya mbolea na upungufu wa virutubisho muhimu kwa mimea.

Sababu nyingine ni pamoja na wakulima kutokuzingatia kanuni bora za kilimo cha kahawa, kutofanya matunzo sahihi ya miti, pamoja na kushindwa kuwekeza ipasavyo katika uboreshaji wa mashamba yao.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Profesa Peter Msofe, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, wakati wa hafla ya ugawaji wa miche bora ya kahawa iliyofanyika katika Kijiji cha Kishimundu, Kata ya Uru Mashariki, Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine zinazoathiri uzalishaji wa kahawa ni uwepo wa miti iliyozeeka, magonjwa na wadudu waharibifu, pamoja na huduma duni za ugani kwa wakulima.

Hata hivyo, alisema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya kahawa ili kuongeza uzalishaji na mchango wake katika uchumi wa taifa.

Alieeleza kuwa juhudi zinaendelea kufanyika kuboresha mazingira ya biashara, kuondoa vikwazo, na kuhakikisha wakulima wanapata bei yenye tija kwa mazao yao.

Aidha, alisema tija ya kahawa kwa wakulima wadogo bado iko chini ikilinganishwa na wakulima wakubwa pamoja na baadhi ya nchi nyingine zinazozalisha zao hilo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, alisema kuwa endapo miche hiyo ya kahawa itasimamiwa vizuri kwa kufuata maelekezo ya maafisa ugani, italeta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa wakulima wa maeneo hayo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Koola, alisema kasi ya ugawaji wa miche ya kahawa bado ni ndogo ikilinganishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi, na kuiomba Bodi ya Kahawa kuongeza juhudi ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.

Baadhi ya wakulima akiwemo Erimina Temba, Dominic Nja, Philemon Njau na Samweli Materu na Patrick Ngowi, wameishukuru serikali kwa kuwapatia miche hiyo ya kahawa wakisema itawasaidia kuongeza uzalishaji na kipato chao.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.