MOSHI-KILIMANJARO.
IMEELEZWA kuwa kahawa inayolimwa katika maeneo ya miinuko ya juu, inasifika kwa ladha bora, harufu nzuri pamoja na uwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa.
Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB),Primus Kimaro, aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa miche elfu 15 ya kahawa, uliofanyika katika kata ya Uru Mashariki, wilayani Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.
Alisema mkoa wa Kilimanjaro umebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba inayofaa kwa uzalishaji wa kahawa bora na kwamba kahawa inayolimwa kwenye miinuko hukua polepole, kutokana na hali ya baridi, jambo linalochangia kupata ladha iliyokolea na yenye ubora wa hali ya juu.
Alisema kahawa ya miinuko ina ubora mkubwa zaidi wa ladha ikilinganishwa na ile inayolimwa katika maeneo ya tambarare.
Akizungumzia historia ya zao hilo, alisema hata kabla ya Uhuru wa Tanzania, kahawa kutoka Uru Mashariki ilikuwa ikipendwa sana na Waingereza.
Aidha, aliongeza kuwa aliyekuwa Malkia wa Uingereza, Elizabeth, alipendelea sana kunywa kahawa kutoka Kilimanjaro, hususan ile iliyolimwa katika eneo la Uru.
"Licha ya kuwepo kwa zaidi ya nchi 50 duniani zinazolima kahawa, kahawa ya Kilimanjaro imeendelea kujitofautisha kutokana na ladha yake ya kipekee."alisema.
Akizungumzia vyama vya ushirika, Kimaryo alisisitiza umuhimu wa wakulima kujiunga na vyama hivyo ili kurahisisha uuzaji wa mazao yao.
Alisema kupitia vyama vya ushirika, wakulima hupata fursa ya kupata pembejeo kama mbolea na pia kunufaika na bei nzuri ya kahawa.
"Serikali imeweka utaratibu wa kuwaunganisha wakulima katika vyama hivyo ili kuongeza tija na kuwawezesha kiuchumi,"alisema Kimaryo.
Kahawa aina ya Arabika hupendelea maeneo ya milimani kama vile Kilimanjaro na Iringa, ambapo kwa pamoja huzalisha zaidi ya asilimia 60 ya kahawa nchini.










