MOSHI-KIKIMANJARO.
SERIKALI ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro imeanza rasmi maboresho ya viwanja vya mpira wa miguu ili kujiandaa kupokea timu zitakazoshiriki michuano ya AFCON 2027, hatua inayolenga kuinua sekta ya michezo na uchumi wa eneo hilo.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano ya CHUI CUP 2026, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema tayari kazi ya kuboresha miundombinu ya michezo imeanza katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) pamoja na Uwanja wa Majengo unaomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
"Maboresho haya yanalenga kuhakikisha viwanja hivyo vinakidhi viwango vitakavyowekwa na wataalamu kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), watakaofanya ukaguzi wa viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya mazoezi ya timu wakati wa mashindano hayo."alisema.
Alisema uwepo wa vituo vya mazoezi Moshi utatoa fursa kubwa kiuchumi kwa wananchi, kwani timu zitakapowasili zitahitaji huduma mbalimbali ikiwemo malazi, chakula na usafiri, hali itakayochochea biashara na kipato kwa wakazi wa eneo hilo.
Aidha, Mnzava alitoa wito kwa wadau wa michezo kuwekeza zaidi katika sekta hiyo ili kusaidia kukuza vipaji vya vijana, ambavyo vinaweza kuwa chanzo cha ajira na kuongeza kipato kwa familia nyingi.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhani Mahanyu, alipongeza kuanzishwa kwa mashindano ya CHUI CUP, akisema yameleta chachu mpya ya maendeleo ya michezo wilayani humo.
Mahanyu alitumia fursa hiyo kuwataka madiwani katika kata mbalimbali kuiga mfano huo kwa kuanzisha mashindano yatakayosaidia kukuza vipaji vya vijana.
Naye Diwani wa Kata ya Njiapanda, John Meela, ambaye pia ni mwanzilishi wa mashindano hayo, alisema lengo kuu la CHUI CUP-2026 ni kutambua na kukuza vipaji vya vijana pamoja na kuwatafutia fursa za maendeleo kupitia michezo.
Alibainisha kuwa mashindano ya mwaka huu yalishirikisha jumla ya timu nane, huku fainali ya kwanza katika historia ya mashindano hayo ikiwakutanisha Njiapanda FC na Makuyuni Sokoni FC. Katika mchezo huo, Njiapanda FC iliibuka bingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.
Meela aliongeza kuwa kupitia mashindano yanayoandaliwa katika ngazi ya kata, wilaya yanalenga kupata wachezaji bora watakaounda timu ya pamoja itakayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini.











