MMOSHI-KILIMANJARO.
SERIKALI imeombwa kutenga fedha kwa ajili ya Tume ya Umwagiliaji katika bajeti ya mwaka 2026/2027, ili kufufua mifereji ya maji ya asili iliyokuwa ikitumiwa na wakulima kwa umwagiliaji wa miche ya kahawa.
Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, alitoa ombi hilo alipokuwa akizungumza na wakulima wa kahawa katika Kata ya Uru Mashariki, Wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, wakati wa hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa miche ya kahawa iliyotolewa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).
Koola alisema kuwa kufufuliwa kwa mifereji hiyo kutasaidia upatikanaji wa maji ya umwagiliaji, hivyo kuzuia miche ya kahawa isikauke na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
“Tunatambua kuwa kahawa inahitaji maji ya kutosha, tunaomba serikali kupitia Wizara husika ifufue mifereji ya asili ili wakulima waweze kupata maji kwa wakati na kuendeleza kilimo hiki muhimu,” alisema Koola.
Aliongeza kuwa wakati Bunge linaendelea kupitia makadirio ya bajeti ya mwaka 2026/2027, ni muhimu fedha zitengwe kwa ajili ya kufufua mifereji hiyo katika kata 26 zilizoko Jimbo la Vunjo na Moshi Vijijini zinazolima kahawa, ili kuimarisha zao hilo la kimkakati.
Koola alisisitiza umuhimu wa kahawa kiuchumi, akieleza kuwa zao hilo ni “dhahabu ya kijani,” ambapo kilo moja huuzwa hadi shilingi 12,000.
Alifafanua kuwa mkulima mwenye miche 540 anaweza kupata hadi shilingi milioni 6 kwa msimu, huku mche mmoja ukiweza kuzalisha hadi kilo tatu na kumwingizia mkulima zaidi ya shilingi milioni 13 kwa msimu.
Aidha, alisema kuwa uhamasishaji wa kilimo cha kahawa umefanyika kwa mafanikio katika majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini, ambapo mahitaji ya miche ni 455,000 kwa Vunjo na 500,000 kwa Moshi Vijijini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, alisema kuwa usimamizi mzuri wa miche ya kahawa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo utaleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wakulima wa maeneo hayo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Moshi, John Meela, aliwataka wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo cha kahawa zinazotolewa na maafisa ugani ili kuongeza tija.
Baadhi ya wakulima Protas Msaki, Philemon Njau na Patrick Ngowi, wameishukuru serikali kwa kuwapatia miche ya kahawa, wakisema zao hilo lina matarajio makubwa ya kuinua uchumi wao.
Hata hivyo, wakulima hao waliiomba serikali kuhakikisha inafufua mifereji ya asili ili kuwawezesha kumwagilia miche hiyo kwa ufanisi.















