NYOKA ALETA TAHARUKI OFISI YA MTENDAJI KATA YA MJIMPYA, WATUMISHI WAIKIMBIA OFISI

MOSHI-KILIMANJARO.

HALI ya taharuki imetanda katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mjimpya, Manispaa ya Moshi, baada ya nyoka mkubwa kuonekana akiingia na kujificha ndani ya ukuta wa jengo hilo, hali iliyosababisha watumishi kushindwa kuendelea na kazi zao kwa hofu ya usalama.

Diwani wa Kata ya Mjimpya, Abuu Shayo, aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025.

Alisema changamoto hiyo inatokana na uchakavu wa jengo la ofisi hiyo, ambapo ukuta wake una ufa mkubwa unaohatarisha usalama wa watumishi na wananchi wanaofika kupata huduma.

Alisema tukio hilo lilibainika wakati wa kikao cha Maendeleo ya Kata (WDC), ambapo alipofika alikuta wajumbe wakiwa nje ya ofisi, mtendaji wa kata alimweleza kuwa walilazimika kutoka nje baada ya nyoka mkubwa kuonekana akiingia kupitia ufa wa ukuta na kupanda hadi darini.

“Wakati mwingine tunapokuwa kwenye vikao vyetu, nyoka huyo hutoka na kuanza kuwachungulia watu, hali hii imetupa hofu kubwa na kushindwa kuendelea na shughuli za kiutendaji kama kawaida,” alisema Shayo.

Diwani huyo ameziomba mamlaka husika kulichukulia suala hilo kwa dharura kwa kufanya ukarabati wa jengo hilo ili kuhakikisha watumishi wanafanya kazi katika mazingira salama na yenye ufanisi.

Mbali na tatizo la nyoka, Diwani Shayo aliwasilisha pia changamoto ya uwepo wa shimo la majitaka katika Shule ya Sekondari Mjimpya, ambalo liliharibika kufuatia mafuriko makubwa ya mvua za mwaka jana.

Alisema maji yalijaa na kusababisha shimo hilo kutitia, hali inayoweka maisha ya wanafunzi hatarini, hasa kipindi hiki kuelekea msimu wa mvua za masika.

“Mwaka jana tulipata mafuriko makubwa yaliyoingia katika shimo hilo na kulisababisha kutitia, kwa sasa ni hatari kwa wanafunzi kwani wanaweza kupita karibu nalo na kuzama, tunaomba lichukuliwe hatua za haraka kabla mvua hazijaanza kunyesha,” alisisitiza.

Aidha, diwani huyo alibainisha kwa changamoyo nyingine ya Zahanati ya Mjimpya nayo inakabiliwa na changamoto ya mafuriko, ambapo maji huingia ndani ya jengo hilo na kuathiri utoaji wa huduma za afya.

Alisema watumishi wa zahanati hiyo hulazimika kusitisha huduma kwa wagonjwa na kujikita katika kuondoa maji na tope yanayoingia kila msimu wa mvua, hivyo, ameomba kujengwa kwa ukuta wa kuzuia maji ili kulinda jengo hilo na kuhakikisha huduma zinaendelea bila usumbufu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwajuma Nasombea, amewaagiza Mkuu wa Idara ya Mazingira na Usafi pamoja na Mkuu wa Idara ya Afya kwenda katika Shule ya Sekondari Mjimpya kukagua shimo la majitaka na kubaini hatua stahiki za kuchukua.

“Baada ya kikao hiki, wakuu wa idara husika waende shuleni kuangalia changamoto ya hilo shimo, kama ni jukumu letu tutalishughulikia mara moja, na kama ni la MUWSA, nitamjulisha Katibu Tawala ili hatua zichukuliwe,” alisema.

Kuhusu tatizo la nyoka katika ofisi ya mtendaji, Mkurugenzi huyo pia alitoa maagizo kwa Idara ya Mazingira na Usafi kuhakikisha wanachukua hatua za haraka kumuondoa nyoka huyo na kushughulikia ufa wa ukuta unaosababisha hatari hiyo.

Hatua hizo zinatarajiwa kurejesha hali ya utulivu na kuhakikisha watumishi na wananchi wanapata huduma katika mazingira salama.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.