MADIWANI MOSHI WALILIA UHABA WA MADAWATI SHULENI, WANAFUNZI WAKAA CHINI

MOSHI-KILIMANJARO.

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wamelalamikia uhaba mkubwa wa madawati katika shule mbalimbali, hali inayowalazimu wanafunzi kukaa kwa kubanana darasani huku wengine wakikosa kabisa sehemu ya kukaa na kulazimika kukaa chini.

Wakiwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika kata zao kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, madiwani hao wamesema changamoto ya madawati ni kubwa na inahitaji hatua za haraka ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu, amesema katika Shule ya Msingi Azimio kuna uhaba mkubwa wa madawati kutokana na ongezeko la wanafunzi.

Alieleza kuwa wanafunzi kadhaa wanalazimika kukaa chini darasani na kuiomba halmashauri kuharakisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kununua madawati 116 yanayohitajika shuleni hapo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kaloleni, Nasibu Mariki, alisema Shule ya Sekondari Msasani imepokea wanafunzi 342 wa kidato cha kwanza kwa mwaka huu wa masomo, hali iliyosababisha upungufu mkubwa wa viti na meza kwa wanafunzi hao.

Naye Diwani wa Kata ya Mjimpya, Abuu Shayo, alisema Shule ya Sekondari Mjimpya inakabiliwa na uhaba wa madawati 150, jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kukosa sehemu ya kukaa wakati wa vipindi.

Diwani wa Kata ya Soweto, Paul Maile, alieleza kuwa mbali na changamoto ya madawati, pia kuna madarasa katika Shule ya Msingi Soweto yaliyoathirika kwa nyufa kubwa na kwa sasa hayatumiki kwa hofu ya kuhatarisha usalama wa wanafunzi. Ameitaka serikali kuona umuhimu wa kujenga madarasa mapya ili kuondoa hatari hiyo.

Akijibu hoja zilizowasilishwa na madiwani katika kikao cha Baraza la Madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 halmashauri imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya sekta ya elimu.

Nasombe alisema fedha hizo, zinazotokana na mapato ya ndani ya halmashauri, zimetengwa kwa kuzingatia maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayotaka halmashauri kutumia mapato yao ya ndani kuboresha sekta ya elimu.

Aidha, aliongeza kuwa fedha hizo pia zitatumika katika miradi mingine ya maendeleo ya elimu, ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari mwaka 2028.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.