WAZIRI MKUU KUTINGA KILIMANJARO, KUKAGUA MIRADI NA KUHUTUBIA WANANCHI

MOSHI-KILIMANJARO.

WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuanza ziara ya siku nne mkoani Kilimanjaro kuanzia Jumatano, Februari 18, 2026, ambapo pamoja na mambo mengine atazungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.

Akitoa taarifa ya ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema Waziri Mkuu ataanza ziara yake wilayani Same kwa kuhutubia mkutano wa hadhara utakaofanyika eneo la Ndungu, kisha kupokea taarifa ya ujenzi wa Barabara ya Same–Mkomazi yenye urefu wa kilomita 36 kwa kiwango cha lami.

Alisema akiwa Same pia atatembelea na kukagua Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Makanya, ambacho ni miongoni mwa vyuo vinavyoimarishwa ili kuendana na dhana ya serikali ya kuboresha elimu ya ufundi nchini.

"Baadaye ataelekea wilayani Mwanga kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mwanga."Alisema RC Babu.

Kwa mujibu wa mkuu  huyo wa mkoa, siku ya Alhamisi Waziri Mkuu atakuwa wilayani Rombo, ambako atakagua ujenzi wa Barabara ya Lower (Lower Road) inayojengwa kwa kiwango cha lami, kisha kuweka jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Mwalimu Stephen Moshi, ambayo tayari imepokea wanafunzi 79.

Akiwa Rombo pia atakagua maendeleo ya Kituo cha Forodha cha Holili mpakani mwa Tanzania na Kenya, pamoja na kuzindua jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.

Siku ya Ijumaa, Dk. Nchemba atatembelea ujenzi wa Barabara ya Mabogini–Kahe–Chekereni wilayani Moshi Vijijini, unaotarajiwa kugharimu Sh bilioni 7.2 kwa kiwango cha lami. 

Pia atazindua jengo jipya la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kabla ya kuingia Moshi Manispaa kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Moshi na Stendi mpya ya kisasa ya Ngangamfumuni, kisha kuhutubia mkutano wa hadhara.

Ziara hiyo itaendelea wilayani Hai, ambako atazindua shule ya Sekondari ya Mbatakero, itakayopunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali wa kilomita tisa kwenda na kurudi shule, ataweka pia jiwe la msingi katika ujenzi wa Barabara ya Boma Ng’ombe–Kikavu Chini yenye urefu wa kilomita 3.5.

RC Babu alisema ziara hiyo itahitimishwa kwa shughuli wilayani Siha, ambapo Waziri Mkuu ataweka jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo la Utawala la Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto (KIDH), na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kilimanjaro, kabla ya kufanya majumuisho ya ziara hiyo Moshi Manispaa siku ya Jumamosi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.