MOSHI-KILIMANJARO.
KIWANDA cha kutengeneza viuatilifu vya mazao cha Plant Biodefenders Ltd kimeongeza uwezo wake wa uzalishaji baada ya kuwekeza katika mitambo mipya ya kisasa yenye uwezo wa kuzalisha hadi lita 5,000 za viuatilifu hai kwa siku, hatua inayolenga kuimarisha sekta ya kilimo na kuongeza upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima nchini.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi wa Plant Biodefenders Ltd, Dk. Never Mwambela, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusiana na mitambo hiyo iliyogharimu kiasi cha sh milioni 300.
Dk. Mwambela alisema, uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kuendelea kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto za wadudu waharibifu wa mazao kwa kutumia viuatilifu vya kibaiolojia vinavyolinda afya ya binadamu na mazingira.
"Tayari tumenunua mitambo mipya ya kisasa kwa thamani ya sh milioni 300, tumeshaifunga inafanya kazi, ambayo ina uwezo wa kuzalisha lita 5,000 za viuatilifu hai kwa siku, tofauti na hapo awali mitambo iliyokuwepo ilikuwa na uwezo wa kuzalisha lita 2,000,"alisema Dk. Mwambela.
Dk. Mwambela, ambaye pia ni mtafiti na mbunifu wa dawa za asili na viuatilifu vya kibaiolojia, alisema kuongezeka kwa uwezo wa uzalishaji kutasaidia kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakulima wa mazao mbalimbali nchini.
Alieleza kuwa viuatilifu vinavyozalishwa na kampuni hiyo vinatumika katika mazao ya parachichi, kahawa, pamba, mpunga, mahindi, korosho, ufuta na mazao mengine muhimu ya biashara na chakula.
“Uwekezaji huu utasaidia kuongeza upatikanaji wa viuatilifu bora kwa wakulima, kuongeza mavuno, kuboresha ubora wa mazao na kupunguza hasara zinazotokana na wadudu waharibifu,” alisema Dk. Mwambela.
Aliongeza kuwa hatua hiyo pia itachangia kukuza uchumi kwa kuongeza fursa za ajira, ambapo zaidi ya ajira 50 za moja kwa moja zinatarajiwa kuzalishwa kiwandani, huku zaidi ya watu 600 wakinufaika kupitia mtandao wa mawakala na wasambazaji wa bidhaa hizo nchini kote.
Kwa mujibu wa Dk. Mwambela, matumizi ya viuatilifu hai yanaendelea kupata umuhimu mkubwa kutokana na mchango wake katika kuendeleza kilimo salama, kuongeza tija na kulinda mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya kemikali za kilimo.
Alisema Plant Biodefenders Ltd itaendelea kufanya tafiti na ubunifu wa bidhaa mpya za kibaiolojia ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto mbalimbali za uzalishaji na kuhakikisha nchi inapata mazao yenye ubora wa juu kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.










