MOSHI-KILIMANJARO.
ROBO fainali ya mashindano ya Zuberi Cup kati ya Green Eagle FC na Kilimanjaro Wonders FC imegubikwa na vurugu na kushindwa kukamilika baada ya mchezo kusimama dakika ya 76, huku Kilimanjaro Wonders ikiwa mbele kwa mabao 3-2 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Railway Njoro, Moshi.
Green Eagle ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza katika dakika ya pili kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Ally Bundala, baada ya beki wa Kilimanjaro Wonders kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Kilimanjaro Wonders haikukaa nyuma, kwani dakika ya 18 ilipata bao la kusawazisha kupitia Fikiri Wasi, aliyefunga moja kwa moja kutokana na mpira wa kutengwa.
Dakika ya 26, Kilimqnjaro Wonders, iligeuza kabisa mchezo kwa kupata bao la pili kupitia Alexander Vicent, kabla ya John Ombeni kuongeza bao la tatu dakika ya 29 na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-1.
Kipindi cha pili Green Eagle ilirejea ikiwa na dhamira ya kusawazisha na dakika ya 47 ikapata bao la pili kupitia Calvin Kishoko, hivyo kupunguza tofauti na kufanya ubao wa matokeo kusomeka Kilimanjaro Wonders 3-2 Green Eagle.
Hata hivyo, dakika ya 76 ndipo mchezo ulipogeuka kuwa wa vurugu baada ya Green Eagle kufanya shambulizi langoni mwa Kilimanjaro Wonders, wakati mpira ukipigwa kwa njia ya krosi, mshambuliaji wa Green Eagle tayari alikuwa amejenga kibanda (kuotea), na hivyo kudai kufanyiwa madhara na kuanza kumfuata mshika kibendera namba moja, ambaye hakuridhia madai hayo, baada ya kunyimwa goli.
Tukio hilo lilisababisha mvutano mkubwa uwanjani, ambapo mshambuliaji huyo wq timu ya Green Eagle alikwenda kumkabili mshika kibendera, huku kocha wa Green Eagle pamoja na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo nao wakihusishwa katika vurugu hizo.
Katika vurugu hizo, kocha wa Green Eagle alilazimika kwenda kumshambulia Katibu wa Mashindano, Iddi Chaku, hali iliyosababisha mchezo kusimama na Jeshi la Polisi kulazimikq kuingia uwanjani kuimarisha usalama.
Polisi waliwalazimika kuwaondoa waamuzi wa mchezo huo uwanjani kwa ajili ya usalama wao, huku hali ikiwa imetawaliwa na mvutano mkubwa baina ya wachezaji, viongozi na mashabiki, ambao hawakuridhika na maamuzi hayo.
Baada ya hali hiyo kutokuwa salama kwa mchezo kuendelea, Kamati ya Mashindano ya Zuberi Cup, iliwatangazia watazamaji kuwa mchezo huo usingeweza kuendelea, wakati Kilimanjaro Wonders ikiwa tayari inaongoza kwa mabao 3-2.
Hatima ya mchezo huo, pamoja na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya waliohusika na vurugu hizo, sasa inasubiri uamuzi wa Kamati ya Mashindano kwa mujibu wa kanuni za Zuberi Cup.








