LA FAMILIA FC YATINGA ROBO FAINALI ZUBERI CUP, MANDELA RANGERS YAAGA

MOSHI-KILIMANJARO.

TIMU  ya La Familia FC imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Zuberi Cup, baada ya kuichapa Mandela Rangers FC mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Railway Njoro, Moshi.

La Familia FC ilianza mchezo huo kwa kasi, ikitafuta bao la mapema na juhudi zake zilizaa matunda dakika ya 11, baada ya mshambuliaji wake mwenye jezi namba 10, Razaki Rasidi, kufunga bao la kwanza na kuifanya timu yake kuongoza.

Hata hivyo, Mandela Rangers FC haikukata tamaa na dakika ya 42 ilipata bao la kusawazisha kupitia Hamad Kibaindo, aliyefunga kwa kichwa kufuatia mpira wa kona, na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa ushindani mkubwa, huku La Familia FC ikiongeza mashambulizi na dakika ya 67 Hamisi Tambwe akaiandikia timu yake bao la pili, kabla ya dakika ya 72 kuibuka tukio lililobadili mwelekeo wa mchezo.

Tambwe alipokuwa akisakama lango la Mandela Rangers FC, alifanyiwa faulo na kipa wa timu hiyo, Nudin Gao, ambaye mwamuzi alimuonyesha kadi nyekundu na kuifanya Mandela Rangers FC kuendelea na mchezo ikiwa pungufu.

Katika dakika ya 82, La Familia FC ilitumia vyema nafasi hiyo na kufunga bao la tatu kupitia Faridi Kubanda, na hivyo kuhitimisha mchezo kwa ushindi wa mabao 3-1 na kupata tiketi ya kucheza robo fainali, huku Mandela Rangers FC ikiondolewa kwenye mashindano hayo.

Mchezo huo ulihudhuriwa na takribani watazamaji 3,000, akiwemo mdhamini wa mashindano hayo, Zuberi Abdallah Kidumo, pamoja na madiwani Khalid Shekoloa wa Kiusha, Alhaji Ally Pendo Dunga wa Msaranga, Haji Fundi wa Bondeni na Issa Elias Bulilo wa Korongoni.

Madiwani hao walishuhudia timu walizokuwa wakiziunga mkono zikiondolewa mapema katika mashindano hayo.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.