MOSHI-KILIMANJARO.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini, Faraji Kibaya Swai, baada ya Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini kutembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Rau kwa lengo la kujionea vivutio mbalimbali na kuhamasisha utalii wa ndani.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Swai amewapongeza wajumbe wa Kamati ya Siasa kwa kutembelea hifadhi hiyo, akisema wamekuwa mabalozi wa utalii ambao wanatarajiwa kuhamasisha makundi mengine ya wananchi kutembelea eneo hilo.
"Utalii wa ndani una umuhimu katika kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi, huku watalii wakichangia mapato ya Taifa na kukuza shughuli za kiuchumi zinazowazunguka wananchi."alisema.
Alisema baada ya kukamilisha ziara ya ukaguzi wa Ilani ya CCM, alipata fursa pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Siasa kutembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Rau, ambako walijionea vivutio ambavyo bado havijatangazwa vya kutosha.
Alisema walitembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo zao la utalii wa kutumia mtumbwi, eneo la malazi ya kitalii (camp site) pamoja na mti wa mvule unaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 200.
Swai alisema miongoni mwa vivutio vilivyomvutia zaidi ni safari ya kutumia mtumbwi hadi kufika katika kisiwa kilichopo ndani ya eneo la maji, akieleza kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kuona kisiwa ndani ya mto.
“Kati ya maeneo ambayo yalinivutia zaidi ni kupanda kwenye mtumbwi hadi tukafikishwa kwenye kisiwa; sijawahi kuona ndani ya mto kukawa na kisiwa, hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza,” alisema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Issa Elias Bulilo, alisema utalii wa ndani una faida mbalimbali, ikiwemo kulitangaza eneo husika, kutambulisha fursa zilizopo na kuongeza mzunguko wa fedha kwa wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao katika maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo.
“Utalii wa ndani una faida nyingi, ikiwemo kutangaza mji wetu wa Moshi, kutangaza fursa tulizonazo katika wilaya yetu na kuongeza uchumi pamoja na kipato cha watu wanaozunguka maeneo ya hifadhi,” alisema Bulilo.
Naye Kaimu Mhifadhi Daraja la Pili kutoka TFS Hifadhi ya Mazingira Asilia Rau, Zayana Mrisho Hashim, alisema Wajumbe hao walipata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali, ikiwemo mti mkubwa wa mvule wenye umri wa miaka 200.
Zayana alisema hifadhi hiyo imeendelea kuibua mazao mapya ya utalii, yakiwemo eneo la malazi (camp site), pamoja na utalii wa kuendesha mtumbwi katika mtiririko wa maji unaohusishwa na vyanzo vya Mto Rau.
Alisema zao la utalii wa kuendesha mtumbwi limechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutangaza vivutio vilivyopo.
“Ndani ya Hifadhi ya Mazingira Asilia Rau tunayo mazao mapya ya utalii, ikiwemo zao la malazi (camp site), ambapo mtalii anaweza kuja na familia yake na kulala kwenye tenti. Pia kuna zao la kutumia mtumbwi katika mtiririko wa maji ya maziwa, ambao ni miongoni mwa vyanzo vya maji vya Mto Rau,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utalii wa ndani, huku akiwapongeza Wajumbe wa Kamati ya Siasa kwa kuunga mkono jitihada hizo kupitia ziara yao katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Rau.
“Kipekee namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiungo katika kuhamasisha utalii wa ndani. Pia nawashukuru Kamati ya Siasa kwa kuunga mkono jitihada hizo na kuja kutembelea hifadhi yetu ya Rau,” alisema Mnzava.






















