MOSHI-KILIMANJARO.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, amemsaidia mwanamke mwenye ulemavu mtaji wa Shilingi 300,000 kwa ajili ya kuendesha biashara ndogo na kujikwamua kiuchumi.
Shayo ametoa msaada huo akieleza kuwa anaendelea kuwa na imani na watu wenye mahitaji maalumu, kwa kuhakikisha wanapata fursa za kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Amesema mwanamke huyo alifika katika ofisi yake Ijumaa, Septemba 18, mwaka huu, akiwa na ombi la msaada, lakini kutokana na muda kuwa mchache, ambapo zilikuwa zimebaki dakika tano kabla ya kwenda msikitini, hakupata nafasi ya kumsikiliza moja kwa moja. Hata hivyo, alimwelekeza Katibu wake kuendelea na mazungumzo naye.
Shayo amesema baada ya kurejea alipatiwa taarifa na Katibu wake kwamba mwanamke huyo alikuwa akiomba msaada wa Shilingi 300,000 kwa ajili ya mtaji wa biashara.
“Nikuombe radhi sana. Mbele ya Naibu Katibu Mkuu hapa laki tatu. Naomba ufi ke hapa mbele nikupatie mbele ya Naibu Katibu Mkuu CCM Bara,” amesema Shayo.
Kwa upande mwingine, Shayo amesema baadhi ya ahadi alizozitoa wakati akiomba ridhaa ya wananchi kumchagua kuwa mwakilishi wao Bungeni, amekuwa akizitekeleza kwa kutumia fedha zake binafsi
Amesema miongoni mwa ahadi hizo ni kununua gari la kubeba wagonjwa, gari la kubeba miili ya marehemu pamoja na magari mawili aina ya Coaster kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii kwa wananchi wa Moshi Mjini.
“Napenda kukutaarifu kwamba kwa kipindi kifupi, ahadi hizo nimezitekeleza kwa kununua vyombo hivyo vya moto vyenye thamani ya Shilingi milioni 300,” amesema Shayo.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Linda Macha amemshukuru Mbunge Shayo kwa kumsaidia mtaji huo, akisema fedha hizo atazitumia kuendesha biashara zake ndogo ndogo ili ziweze kumsaidia kujikwamua kiuchumi.
Macha amesema Shayo amekuwa akitoa msaada kwa makundi mbalimbali bila ubaguzi, likiwamo kundi la watu wenye ulemavu, jambo alilosema linawapa matumaini na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii






