MOSHI-KILIMANJARO.
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Foundation for Community Transformation in Kilimanjaro (FTK), linalojihusisha na shughuli za maendeleo ya jamii, limekabidhi madawati 114 yenye thamani ya Sh milioni 17.6 kwa shule za msingi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Madawati hayo yamegawiwa katika shule nne za msingi, ambapo Shule ya Msingi Mawala imepokea madawati 33, Mkalama madawati 31, huku shule za Miwaleni na Kisangesangeni kila moja ikipokea madawati 25.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati 25 katika Shule ya Msingi Kisangesangeni, Mratibu wa Miradi wa FTK, Frank Mihayo, amesema wameamua kutoa msaada huo baada ya kubaini changamoto kubwa ya upungufu wa madawati katika shule hiyo, hali iliyokuwa ikiwalazimu wanafunzi kukaa kwa kubanana.
Amesema licha ya Serikali kujenga madarasa mawili mapya katika shule hiyo, bado kulikuwa na changamoto ya madawati, hivyo shirika hilo likaona umuhimu wa kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa msaada huo ili kupunguza adha inayowakabili wanafunzi.
Mihayo amesema msaada huo pia umefika katika Shule ya Msingi Miwaleni, ikiwa ni mwendelezo wa shirika hilo kusaidia shule zilizopo Kata ya Arusha Chini na maeneo mengine yanayozunguka shamba la miwa la TPC, ambako FTK inatekeleza shughuli zake za maendeleo ya jamii.
Aidha, amesema shirika hilo limekabidhi magunia ya mahindi na maharage kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kahe Magharibi, Abdul Msangi, ameishukuru FTK kwa msaada huo, akisema utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza changamoto iliyokuwa ikiwasababisha baadhi ya wanafunzi kukaa kwa kubanana na wengine kulazimika kupokezana zamu za kukaa.
Msangi amesema FTK imekuwa ikitoa msaada kwa shule hiyo, ambapo awali ilikabidhi madawati 25 na sasa imeongeza mengine 25.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia shule za msingi za serikali zilizopo katika kata hiyo, ambazo bado zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati.
Amezitaja shule zinazohitaji msaada huo kuwa ni Mwangaria, Kahe, Mawala, Oria, Rau River na Maendeleo, akisema changamoto hiyo inahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kisangesangeni Emmanuel Mrema, amesema shule hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati 60 na kuishukuru FTK kwa kuendelea kuisaidia shule hiyo, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto iliyokuwa ikiathiri ustawi wa wanafunzi na mazingira ya kujifunzia.








