MOSHI-KILIMANJARO.
WAKAZI wa Kata ya Msaranga, Manispaa ya Moshi, wameiomba Serikali kutenga eneo maalumu kwa ajili ya makaburi ya jamii, wakieleza kuwa wanakabiliwa na changamoto ya kukosa eneo rasmi la kuzikia ndugu zao wanapofariki dunia.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Diwani wa kata hiyo, Alhaji Ally Pendo Dunga, kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, wamesema kukosekana kwa eneo la makaburi kumewalazimu baadhi yao kuzikia ndugu zao katika maeneo ya makazi, huku wengine wakizuiwa kufanya hivyo.
Mkazi wa kata hiyo, Felex Njau, amesema aliwahi kufiwa na baba yake mdogo na kuzuiwa kumzika katika eneo la nyumbani kwao, huku akidai kuwa jirani yake aliyepatwa na msiba aliruhusiwa kuzika nyumbani bila kuzuiwa.
“Mimi nilifiwa na baba yangu mdogo, nilizuiliwa kumzika nyumbani, lakini kuna jirani yangu alipofiwa alizika nyumbani kwake na hakukuwa na mtu aliyefika kumzuia, kama ni kuzika nyumbani, basi watu wote waruhusiwe bila kujali uwezo wao wa kifedha,” amesema Njau.
Mkazi mwingine wa kata hiyo Ntipas amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha malalamiko miongoni mwa wananchi, wakidai kuwa baadhi ya watu wenye uwezo wa kifedha wamekuwa wakiruhusiwa kuzika ndugu zao katika maeneo yao ya makazi, wakati wale wasio na uwezo wakikumbana na vikwazo wanapojaribu kufanya hivyo.
Akijibu malalamiko hayo, Diwani wa Kata ya Msaranga, Alhaji Ally Pendo Dunga, amesema kwa mujibu wa Sheria za Mipango Miji, wananchi hawaruhusiwi kuzika ndugu zao katika maeneo ya makazi, badala yake wanapaswa kutumia makaburi yaliyotengwa na Serikali, ikiwamo eneo la Karanga.
Aidha diwani huyo, amesema kata hiyo inakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa eneo maalumu la makaburi kutokana na uhaba wa ardhi, huku maeneo mengi yakiwa tayari yametumika kwa makazi ya wananchi.








