TIDI YAPONGEZWA KWA MAPAMBANO DHIDI YA KIFUA KIKUU SUGU

SIHA-KILIMANJARO.

SERIKALI wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro, imeipongeza Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI) kwa mchango wake katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, hususan kifua kikuu na kifua kikuu sugu, kupitia huduma za kibingwa, uchunguzi na matibabu.

Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka, ametoa pongezi hizo Novemba 6,2026 wakati akizindua wiki ya uchunguzi na matibabu ya afya bila malipo kwa wananchi, hafla iliyofanyika katika viwanja vya taasisi hiyo wilayani humo.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu huyo wa wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha, Jane Chalamila, amesema kuanzishwa kwa TIDI kumeongeza uwezo na wigo wa taifa katika utoaji wa huduma za kibingwa, uchunguzi, utafiti, mafunzo pamoja na mwitikio dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.

Chalamila amesema huduma zinazotolewa na taasisi hiyo ni muhimu kwa wananchi, hivyo amewahimiza wakazi wa Siha na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ya kupata uchunguzi na matibabu bila malipo, badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata baadhi ya huduma hizo.

Aidha, ameipongeza menejimenti ya TIDI inayoongozwa na Mkurugenzi wake, Dk. Leonard Subi, kwa uongozi wenye maono, ubunifu na usimamizi madhubuti, akisema katika miaka ya hivi karibuni taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika kuboresha miundombinu, huduma na uwezo wa kitaalamu.

"Katika kuadhimisha miaka 100 ya taasisi hii, TIDI imeamua kuadhimisha kwa kushirikiana na jamii kupitia wiki maalumu ya uchunguzi, upimaji na matibabu bila malipo, inayofanyika kuanzia Novemba 5 hadi 8 mwaka huu."amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TIDI, Dk. Leonard Subi, amesema wiki hiyo imeandaliwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za uchunguzi kutoka kwa madaktari bingwa, ushauri wa kitaalamu na matibabu.

Ameongeza kuwa wagonjwa watakaobainika kuwa na changamoto zinazohitaji uangalizi zaidi wataunganishwa na vituo vinavyoweza kuwapatia huduma hizo.

Naye Mratibu wa Kifua Kikuu Sugu wa TIDI, Dk. Happiness Mvungi, amesema katika kambi hiyo ya siku nne, wananchi watapata huduma mbalimbali zikiwemo za magonjwa ya ndani, mfumo wa mkojo, ngozi na mifupa.

Kambi hiyo imewashirikisha madaktari bingwa na wabobezi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Hospitali ya Mount Meru, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi, Hospitali ya Wilaya ya Siha pamoja na wataalamu kutoka TIDI, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.























Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.