TIDI YAWAPELEKA WALIOPONA TB SUGU KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII KAMA SEHEMU YA TIBA

 SAME-KILIMANJARO.

WAGONJWA waliopona ugonjwa wa Kifua Kikuu Sugu (TB Sugu) wanaopatiwa huduma katika Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Tanzania (TIDI), wamepelekwa kutembelea vivutio vya utalii wa ndani, ikiwa ni sehemu ya matibabu ya kisaikolojia yanayolenga kuwaimarisha afya ya akili kabla ya kurejea katika familia na jamii zao.

Ziara hiyo iliwahusisha wagonjwa15 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar walitembelea Chemka Hot Springs, iliyopo Kijiji cha Rundugai, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kuwapa fursa ya kubadilisha mazingira, kupata utulivu wa akili, kujifunza kuhusu vivutio vya asili na kuchangamana na watu wengine.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa Ustawi wa Jamii wa TIDI, Wazoeli Mshana, amesema utaratibu huo ni sehemu ya programu ya afya ya akili inayolenga kuwaandaa wagonjwa waliopona TB sugu kurejea katika jamii baada ya kukaa kwa muda mrefu katika taasisi hiyo wakipatiwa matibabu.

Amesema wagonjwa hao hukaa TIDI kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita, hali inayoweza kuwafanya baadhi yao kupata sonona na majonzi kutokana na kutengana na familia zao, hivyo ziara za kutembelea maeneo ya utalii zimekuwa msaada katika kuwapa faraja, utulivu na kuwaandaa kisaikolojia kabla ya kurejea nyumbani.

Mshana amesema programu hiyo ilianza mwaka 2022 baada ya taasisi hiyo kuona umuhimu wa kuwaongezea wagonjwa huduma za afya ya akili, ambapo Shirika la LHL International kutoka nchini Norway lilikubali kufadhili utaratibu huo, ambao sasa umefikia mwaka wa nne wa utekelezaji.

Amesema tangu kuanzishwa kwake, wagonjwa hao wamekuwa wakitembelea maeneo mbalimbali yakiwamo Hifadhi za Taifa za Tarangire, Arusha na Mkomazi, Bustani ya Wanyama ya Siha, huku safari ya hivi karibuni ikiwa ni kutembelea Chemka Hot Springs ili kujionea na kujifunza kuhusu maji ya asili yanayotoka chini ya ardhi.

Ameongeza kuwa utaratibu huo hufanyika baada ya wataalamu wa afya kuwafanyia wagonjwa vipimo na kuthibitisha kuwa wamepona na hawana maambukizi tena, ambapo ziara hizo huwapa nafasi ya kufurahia mazingira ya asili na kuimarisha afya yao ya akili kabla ya kukamilisha taratibu za kurejea katika mikoa wanayotoka.

Kwa upande wake, Dk. Julius Kahenja kutoka Idara ya TB Sugu (MDR), amesema takwimu za taasisi hiyo zinaonesha kuwa asilimia 75 ya wagonjwa wa TB sugu wanaofikishwa TIDI kwa matibabu hupona, akieleza kuwa kuwapeleka waliopona kutembelea vivutio vya utalii ni sehemu ya kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida baada ya kukaa muda mrefu hospitalini.

Amesema wagonjwa hao hutumia muda mrefu wakiwa kwenye matibabu na kupumzika vitandani, hivyo kuwatoa katika mazingira hayo na kuwapeleka maeneo ya utalii kunawapa fursa ya kupata uzoefu mpya, kufurahia mazingira na kujenga upya hali yao ya kisaikolojia.

Baadhi ya wagonjwa walioshiriki ziara hiyo, akiwamo Zuena Ramadhan Swalehe kutoka Kibaha mkoani Pwani, Joseph Jonathan Mgaya kutoka mkoani Njombe, Alexs Nicholas Lyaswai kutoka Rombo na Rock Perer Shempemba kutoka mkoani Tanga, wameishukuru TIDI kwa kuanzisha utaratibu huo, wakisema umewapa nafasi ya kutembelea maeneo ambayo baadhi yao hawakuwahi kuyafika.

Wamesema mbali na kujionea uzuri wa Chemka Hot Springs, ziara hiyo imewapa furaha, nafasi ya kuchangamana na wenzao na kushiriki shughuli za burudani ikiwamo kuogelea, hali wanayoieleza kuwa imewasaidia kupata faraja na kuondoa mawazo baada ya kipindi kirefu cha matibabu.




















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.