WAZAZI WATAKIWA KUENDELEA KUSIMAMIA MALEZI YA WATOTO HATA BAADA YA KUHITIMU SHULE

SAME-KILIMANJARO.

WAZAZI wametakiwa kuimarisha usimamizi wa watoto na kuwajengea misingi imara ya maadili, nidhamu na uwajibikaji, si tu wanapokuwa shuleni, bali hata baada ya kuhitimu masomo na kuingia katika jamii, ili kuwaepusha na changamoto zinazoweza kuathiri maisha na mustakabali wao.

Wito huo umetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT), Stevie Mulenga, wakati wa mahafali ya tano ya wanafunzi wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari New Dawn, iliyopo wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.

Askofu Mulenga amesema jukumu la mzazi halipaswi kuishia mtoto anapohitimu shule au kuanza kujitegemea, bali linapaswa kuendelea kwa kumshauri, kumfuatilia na kumsaidia kufanya maamuzi sahihi yatakayolinda maisha yake.

Amesema kuhitimu shule ni mwanzo wa safari nyingine ya maisha yenye changamoto nyingi zinazohitaji busara na maamuzi sahihi, akiwataka vijana kutambua kuwa kuvua sare za shule hakumaanishi kuachana na nidhamu waliyojengewa kwa kipindi chote cha masomo.

“Unapovua sare za shule na kuvua nidhamu, umeanza utupu wa maisha. Sare ni kitambaa unachoweza kukivua, lakini nidhamu ni tabia uliyoivaa kwa miaka minne. Ukiivua, unabaki mtupu na maisha ya nje duniani huko hayana huruma kwa mtu asiye na maadili,” amesema.

Ameeleza kuwa wanapokuwa shuleni wanafunzi hulindwa na mambo manne ambayo ni sare, kengele, walimu na uzio wa shule, lakini baada ya kuhitimu wanapaswa kujisimamia wenyewe kwa kutumia misingi ya nidhamu waliyojengewa.

Aidha, amewataka vijana kuwa makini katika kuchagua marafiki, kuepuka kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi wakiwa bado hawajajipanga kimaisha, kutumia simu na mitandao ya kijamii kwa manufaa, pamoja na kujifunza kujitegemea, kufanya kazi na kuweka akiba.

Pia amewataka kutokubali kutawaliwa na hofu, tamaa, tabia ya kujilinganisha na wengine wala kukata tamaa wanapokutana na changamoto, akisisitiza kuwa mafanikio yanahitaji uvumilivu, bidii na maamuzi yenye tija.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa shule hiyo, Dk. Stephen Mshomi, amewataka wazazi kuendelea kutekeleza wajibu wao wa malezi hata baada ya watoto kuhitimu Kidato cha Nne, Kidato cha Sita au kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

Amesema baadhi ya changamoto za kitabia zinazowakabili vijana katika jamii zinachangiwa na wazazi kushindwa kutekeleza ipasavyo wajibu wao wa kuwaongoza na kuwafuatilia watoto katika hatua mbalimbali za ukuaji wao.

Naye Mwenyekiti wa Wazazi wa shule hiyo, Zakayo Mosha, amewataka wazazi kuwapokea na kuendelea kuwalea vizuri watoto wanaporejea nyumbani baada ya kuhitimu masomo, huku akiiomba Serikali na wadau wa elimu kuisaidia shule hiyo kupanua wigo wa utoaji elimu kwa kuanzisha Kidato cha Tano na Sita pamoja na taasisi ya sayansi na teknolojia.

Amesema shule hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa watoto yatima na wanaotoka katika familia zisizojiweza kwa kuwapatia fursa ya kupata elimu ya sekondari bila malipo, hivyo upanuzi wa huduma zake utaongeza fursa kwa watoto wengi zaidi.

Akitoa taarifa ya shule, Mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Kitadu, amesema jumla ya wanafunzi 38 wamehitimu Kidato cha Nne, huku akieleza kuwa taasisi hiyo inatoa elimu bure kwa watoto yatima, watoto wanaotoka katika mazingira magumu na familia zisizojiweza.

Amesema pamoja na elimu, shule hiyo huwapatia wanafunzi chakula, malazi na mahitaji mbalimbali ya shule, huku ikiweka mkazo katika kuwajengea misingi ya kiroho, kitaaluma, maadili na nidhamu kwa lengo la kuwaandaa kuwa watu wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.

















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.