MOSHI-KILIMANJARO.
![]() |
BODI ya Maji Bonde la Pangani, imezindua muongozo maalumu wa uundwaji wa Jumuiya za Watumia Maji, unaolenga kuweka utaratibu unaofanana katika kuanzisha jumuiya hizo ili kuimarisha usimamizi, uhifadhi na ulinzi wa vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali ya bonde hilo.
Akizungumza wakati wa kikao kilichowakutanisha wenyeviti wa Jumuiya za Watumia Maji 26 zilizopo ndani ya Bonde la Pangani, Mkurugenzi wa PBWB, Mhandisi Segule Ally Segule, amesema muongozo huo umeandaliwa baada ya kubainika kuwepo kwa tofauti na maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika namna jumuiya hizo zinavyoanzishwa na kutekeleza majukumu yake.
Amesema jumuiya hizo ni vyombo muhimu vinavyosaidia Bodi ya Maji Bonde la Pangani kutekeleza majukumu yake katika ngazi ya jamii, hivyo kuwepo kwa muongozo huo kutasaidia kuhakikisha uundwaji wake unazingatia vigezo na taratibu zinazofanana.
Amesema pamoja na uzinduzi huo, wenyeviti wa jumuiya hizo wamepewa jukumu la kusimamia uundwaji wa jumuiya mpya katika maeneo yao na kuwasilisha taarifa kwa bodi ili kufuatilia kama taratibu na vigezo vilivyowekwa vinazingatiwa.
Ameongeza kuwa kikao hicho pia kililenga kuwapa nafasi viongozi hao kueleza fursa na changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, ametoa wito kwa watu wote wenye vibali vya kutumia maji kutoka Bonde la Pangani kujiunga na jumuiya hizo na kutekeleza masharti yaliyokubaliwa, ikiwemo kuchangia gharama za uendeshaji, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni wajibu unaosaidia kuhakikisha usimamizi wa rasilimali hiyo unakuwa endelevu.
Kwa upande wao, baadhi ya wenyeviti wa jumuiya hizo, akiwemo Gaudencia Shirima wa Jumuiya ya Watumia Maji ya Kidakio cha Mto Tarakea na Filipo Yusuph Mdoe wa Jumuiya ya Watumia Maji Zigi Juu;
Wamesema wanakabiliwa na changamoto za uvamizi wa maeneo ya vyanzo vya maji kwa shughuli za uchimbaji madini pamoja na ukataji miti, hali inayohitaji ushirikiano wa jamii katika kulinda maeneo hayo.








