KAMATI ya Mashindano ya Zuberi Cup imeiondoa timu ya Green Eagle FC katika mashindano hayo baada ya wachezaji wake kumpiga mwamuzi wa pembeni katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Kilimanjaro Wonders FC.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Zuberi Cup, Japhet Mpande, ambaye amesema uamuzi huo umefikiwa kutokana na vurugu zilizotokea uwanjani Agosti 11, 2026 ambapo wachezaji wa Green Eagle FC walikwenda kumvamia mwamuzi wa pembeni Agness Mhando na kuanza kumshambulia.
Mpande amesema vurugu hizo zilitokea dakika ya 76 ya mchezo, baada ya Green Eagle FC kufunga bao ambalo lilikataliwa na mwamuzi wa pembeni kwa sababu mshambuliaji wa timu hiyo alikuwa katika nafasi ya kuotea.
Amesema baada ya uamuzi huo, baadhi ya wachezaji wa Green Eagle FC walimvamia mwamuzi wa pembeni na kumpiga, hali iliyosababisha mchezo kusimama na kuibua vurugu kubwa uwanjani.
Katika tukio hilo, kocha wa Green Eagle FC pamoja na baadhi ya mashabiki nao walihusishwa katika vurugu, huku hali hiyo ikilazimisha Jeshi la Polisi kuingia uwanjani kwa ajili ya kuimarisha usalama na kuwaondoa waamuzi wa mchezo huo.
Kabla ya vurugu hizo, Green Eagle FC ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya pili kupitia Ally Bundala kwa mkwaju wa penalti, baada ya beki wa Kilimanjaro Wonders kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Kilimanjaro Wonders ilisawazisha dakika ya 18 kupitia Fikiri Wasi kwa mpira wa kutengwa, kabla ya Alexander Vicent kuongeza bao la pili dakika ya 26. John Ombeni aliifungia timu hiyo bao la tatu dakika ya 29 na kuifanya kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-1.
Kipindi cha pili Green Eagle FC ilirejea kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 47 kupitia Calvin Kishoko, hivyo kufanya matokeo kuwa Kilimanjaro Wonders 3-2 Green Eagle FC.
Hata hivyo, mchezo huo haukuweza kukamilika baada ya kuzuka kwa vurugu dakika ya 76, ambapo Kamati ya Mashindano ililazimika kuusimamisha mchezo huo kwa sababu za kiusalama.
Kwa uamuzi huo, Green Eagle FC imeondolewa katika mashindano ya Zuberi Cup, huku hatua zaidi dhidi ya waliohusika na vurugu hizo zikitarajiwa kuchukuliwa kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo.





