SHIRIKA la Posta Tanzania limewataka Mameneja wake wa mikoa nchini kuwa wabunifu zaidi katika utendaji wa kazi na kutafuta masoko mapya ya huduma ili kuongeza mapato na kuimarisha uwezo wa shirika kujiendesha katika mazingira ya ushindani wa kibiashara.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania, CPA Poniwoa Mbisse, aliyasema hayo Juni 4,2026, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro,alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kukamilisha ziara yake ya kikazi mkoani humo.
CPA Mbisse alisema Shirika la Posta nchini, limejiwekea mikakati mbalimbali ya kufanikisha malengo ya mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwa ni pamoja na Mpango Mkakati wa Miaka Tisa, hivyo Mameneja wanapaswa kuhakikisha wanatumia ubunifu katika kutekeleza majukumu yao ili kufikia malengo hayo.
Alisema kuwa ushindani katika sekta ya huduma za Posta na usafirishaji unazidi kuongezeka, jambo linalohitaji viongozi wa shirika katika ngazi zote kutafuta mbinu mpya za kuvutia wateja na kupanua wigo wa huduma zinazotolewa.
Aidha, alipongeza Meneja wa Posta Mkoa wa Kilimanjaro kwa usimamizi mzuri wa shughuli za shirika, hali iliyochangia kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato pamoja na kusimamia kwa ufanisi miradi ya maboresho ya majengo ya Posta.
CPA Mbisse pia aliwataka mameneja kuongeza juhudi katika kutafuta masoko mapya, kuimarisha huduma kwa wateja na kuhakikisha shirika linaendelea kuongeza tija, mapato na faida.
Awali akitoa taarifa ya utendaji wa shirika mkoani humo, Meneja wa Shirika la Posta Mkoa wa Kilimanjaro, Abubakar Athuman Jangufua, alisema katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha, kuanzia Januari hadi Machi, mkoa ulipangiwa kukusanya mapato ya Sh milioni 257, lakini uliweza kukusanya Sh milioni 321, sawa na asilimia 125 ya lengo.
Aliongeza kusema kuwa Shirika la Posta Kilimanjaro imeanzisha huduma mpya ya SWIFTPACK, ambayo inalenga kuboresha huduma za usafirishaji na ugawaji wa vifurushi na bidhaa kwa kutumia mfumo wa kisasa wa usafiri, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma na mapato ya shirika.
![]() |
![]() |
![]() |











