MIEMBENI-MOSHI.
MAMA mmoja mkazi wa Kata ya Miembeni, Manispaa ya Moshi, ambaye amekuwa amelala kitandani kwa takribani miaka minane kutokana na kupooza kwa sehemu ya mwili wake, ameanza kuona matumaini mapya baada ya kupatiwa matibabu na kiti mwendo na Kituo cha Afya cha Jaffery kinachotoa huduma kwa misingi ya hisani.
Mwenyekiti wa Bodi ya kituo hicho, Salim Mohamed Khaki, amesema waliguswa na hali ya mama huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa Diwani wa Kata ya Miembeni, Haruna Ally Mushi, na kuamua kumsaidia kwa kumpatia kiti mwendo pamoja na kuanza matibabu yake.
Amesema baada ya kupokea taarifa kutoka kwa diwani huyo, alifika nyumbani kwa mama huyo kujionea hali yake na kubaini kuwa alikuwa ameishi maisha ya mateso kwa muda mrefu bila uwezo wa kutoka nje ya nyumba yake.
Aidha, ametoa wito kwa watoa huduma za afya pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu badala ya kutanguliza maslahi ya kifedha.
Kwa upande wake, mama huyo, Mwanaidi Husen Masiki, amesema msaada huo umemrejeshea matumaini baada ya kutumia miaka minane akiwa hawezi kutoka nje bila kubebwa.
Mama huyo amebainisha kuwa baada ya kufanyiwa uchunguzi wa awali katika kituo hicho cha afya, amegundulika kuwa na tatizo la figo na ameshauriwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC kwa ajili ya vipimo vya kina.
Hata hivyo, amesema ameshindwa kuendelea na hatua hiyo kutokana na ukosefu wa fedha za kugharamia vipimo vinavyohitajika, akieleza kuwa anatakiwa kutoa zaidi ya Sh400,000 ili kuendelea na uchunguzi na kuomba msaada zaidi ili aweze kupata vipimo vya mgongo vinavyohitajika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC.
Akizungumza mjukuu wake, Ramadhan Omari, amesema ugonjwa wa bibi yake umekuwa na athari kubwa kwa familia, ikiwemo yeye kulazimika kusitisha masomo kwa muda ili kusaidia kutafuta mahitaji ya msingi ya nyumbani.
Naye Diwani wa Kata ya Miembeni, Haruna Ally Mushi, amepongeza uongozi wa Kituo cha Afya cha Jaffery kwa moyo wa kujitolea kusaidia wenye uhitaji na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana kusaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto za kiafya.












