WASIRA; AAGIZA SAUWASA KUTATUA KERO YA MAJI SAME

SAME-KILIMANJARO


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Stephen Wasira, ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Same (SAUWASA) kuhakikisha inatatua kwa haraka changamoto ya upatikanaji wa maji inayowakabili wananchi wa mji wa Same.

Wasira alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na Wanachama wa CCM wa Shina Namba 9, tawi la Same, Kata ya Same, Wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Akijibu malalamiko ya wananchi kuhusu ukosefu wa maji, alisema haikubaliki kwa wakazi wa Same kuendelea kukosa huduma hiyo muhimu wakati maji yanapatikana kwa wingi kupitia miradi iliyotekelezwa na Serikali.


“Ninaiagiza SAUWASA kuhakikisha wananchi wa Same wanapata maji. Haiwezekani watu wa Same waendelee kuyasikia au kuyaona maji bila kuyapata kwa matumizi yao ya kila siku, mfumo wa usambazaji uharakishwe ili wananchi wanufaike na huduma hiyo muhimu,” alisema Wasira.

Alibainisha kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Same–Mwanga–Korogwe, hivyo hakuna sababu ya wananchi kuendelea kukosa huduma hiyo kutokana na changamoto za usambazaji.

“Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya mradi huu na kwa sasa maji yapo, haitakuwa na maana yoyote kama maji hayo yatakuwepo lakini wananchi wanaolengwa hawawezi kuyapata,” alisisitiza.

Kuhusu maelezo yaliyotolewa kwamba miundombinu ya zamani ya mabomba ndiyo chanzo cha tatizo hilo, Wasira alisema changamoto hiyo inaweza kushughulikiwa na kutatuliwa kwa haraka ili wananchi waondokane na adha ya kukosa maji.

Katika hatua nyingine, Wasira alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mashina ya CCM, akieleza kuwa ndiyo msingi mkuu wa uhai na nguvu ya chama hicho.

Alisema CCM ni chama cha wanachama wake na si cha mtu mmoja, huku akibainisha kuwa mafanikio ya chama yanategemea utendaji kazi wa mashina katika kusikiliza na kuwasilisha kero pamoja na maoni ya wananchi.

“Katika chama chetu, mashina yakishindwa kufanya kazi yake, chama hakiwezi kuwa imara, msingi wa CCM ni mashina, ndiko wananchi wanapopata nafasi ya kueleza matatizo yao na kuyawasilisha katika ngazi mbalimbali za chama,” alisema.


Aidha, aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kuhakikisha mashina yanafanya mikutano mara kwa mara, akieleza kuwa uhai wa chama unategemea mikutano na ushiriki wa wanachama katika kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.

Pia alisisitiza umuhimu wa wanachama kulipa ada za uanachama, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha shughuli na maendeleo ya chama kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.