CCM MWANGA YAKEMEA VIKALI UWEPO WA MAKUNDI YANAYOWAGAWA WANACHAMA

MWANGA-KILIMANJARO.


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mwanga kimeendelea kukemea vikali uwepo wa makundi yanayowagawa wanachama ndani ya chama hicho, kikisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano katika kuimarisha chama na kutanguliza maslahi ya wananchi badala ya maslahi binafsi.

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu wa CCM Wilaya ya Mwanga, Mwadawa Omari Maulid, wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM wa Kata ya Toroha katika mkutano wa kutoa shukrani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka 2025.

Amesema kuwa uwepo wa makundi wakati wa uchaguzi ni jambo la kawaida kutokana na demokrasia ya ndani ya chama, ambapo wagombea mbalimbali huwa na wafuasi wao, hata hivyo, amesisitiza kuwa mara baada ya uchaguzi kumalizika, wanachama wote wanapaswa kuungana na kubaki katika kundi moja la CCM.

“Makundi wakati wa uchaguzi yanaruhusiwa kwa sababu ya ushindani wa kidemokrasia ndani ya chama, kila mgombea huwa na wafuasi wake, lakini baada ya uchaguzi tuna wajibu wa kuyaondoa makundi yote na kubaki na kundi moja la CCM,” alisema.

Aliongeza kuwa jukumu la viongozi na wanachama wa CCM kwa sasa ni kuisimamia Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake na kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na maendeleo yanayoletwa kupitia Ilani ya CCM.

“Uchaguzi umekwisha, tuachane na makundi ya uchaguzi na tujielekeze katika kujenga chama na kuwatumikia wananchi, bado kuna baadhi ya maeneo ambayo watu hawawezi hata kuthamini maendeleo yanayoletwa kwa sababu ya kuendelea kushikilia makundi ya uchaguzi,” alisema.

Katibu huyo alisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni nguzo muhimu zitakazokiwezesha chama kuendelea kutekeleza kwa ufanisi ahadi zake kwa wananchi na kuimarisha maendeleo katika jamii.

Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Jeremiah Boniphace Mziray, amewataka wananchi kuendelea kumpa ushirikiano Mbunge wao, Dk. Ngwaru Maghembe, akieleza kuwa tayari ameanza kutekeleza ahadi mbalimbali alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Alisema baadhi ya miradi ya maendeleo imeanza kutekelezwa katika kata mbalimbali za jimbo hilo, jambo linalodhihirisha dhamira ya mbunge huyo katika kuwatumikia wananchi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga, Ibrahim Mnzava, amesema ushindi wa Dk. Ngwaru Maghembe katika uchaguzi mkuu mwaka 2025, haukuwa wa bahati mbaya, bali ulitokana na imani kubwa ya wananchi kwa CCM na utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.

Mnzava alisema ushindi huo ni ishara ya kuridhishwa kwa wananchi na kazi zinazofanywa na CCM pamoja na Serikali yake katika kuwaletea maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.