NA KIJA ELIAS, MOSHI
WAKATI wazungu wanagawana bara la Afrika kupitia Mkutano Mkuu wa Berlin mnamo mwaka 1884, Otto Van Bismarck ndiye aliyesimamia mkutano huo. Tanganyika ilichukuliwa na Wajerumani waliotawala hadi walipopigwa laza na Waingereza 1918.
Wajerumani walipokuja walikuta baadhi ya maeneo kuna tawala zenye nguvu, zilizokua na mfumo rasmi wa uongozi. Wachaga ni miongoni mwa tawala zilikuwa na mfumo rasmi wa uongozi na walikuwapo pembezoni mwa mlima Kilimanjaro kuanzia maeneo ya Rongai hadi Siha. Eneo hili lilikua na mtawala mkuu mmoja (aliyeitwa Mangi Mkuu). Huyu alikuwa kama Rais ama Mfalme wa jamii hiyo.
Mangi Rindi Mandara alikuwa mtawala wa Moshi kutoka mwaka 1860 hadi 1891. Huyu alikuwa baba wa Meli aliyekuja kukalia kiti cha baba yake. Kwenye maisha yake Rindi Mandara alikuwa mwana diplomasia mzuri hasa katika kutunza mahusiano mazuri baina yake na machifu wengine wa Kilimanjaro.
Alikuwa mtaalamu wa kusimamia mahusiano ya kitaifa kati ya Wajerumani ambayo kipindi hicho yalikuwa katika hali mbaya. Alitumia ujuha wa wakoloni hao kutoka Ulaya ambao hawakuelewa lolote kuhusu Uchagani, kuboresha maisha na kuipa fursa jamii ya kijijini mwake.
Mnamo mwaka 1889 mabalozi wanne walisafiri kwenda Ujerumani kukutana na Kaiser ambao ni Ndasha, Ndengarisha, Ndura na Ravira. Katika maandiko ya Kijerumani inaelezwa kuwa wachaga hawa walipofika huko hawakupenda kabisa kupigwa picha na mmoja kati yao alikataa kata kata kupigwa picha tena kwa matamshi.
Baada ya kifo cha Rindi Mandara, Meli alikalia kiti cha baba yake. Mangi Meli alikuwa tofauti kidogo na baba yake. Roho ya umoja iliyotumiwa na Wachaga kwenye mapambano yao dhidi ya ukoloni kipindi wakishambuliwa na majeshi ya Kijerumani ilimuwezesha Mangi Meli kupata ushindi mkubwa mnamo mwaka 1892. Wajerumani walilazimika kukimbia na kusitisha utawala wao katika eneo la Moshi takribani mwaka mmoja.
Waliporudi katika ardhi hiyo walifanikiwa kuzima ndoto za Wachaga wa Moshi kuwa dola kubwa ambapo Wajerumani walijenga boma ambalo liliharibiwa mnamo mwaka 1893 baada ya Mangi Meli kutoa upinzani tena.
Nyumba mpya ya Mangi Meli ilijengwa juu ya mlima ikitazama mizinga ya Wajerumani, hatua hiyo iliimaanisha utawala wa Mangi Meli ulikuwa ukielekea mwisho. Wakati wa mapambano yake dhidi ya majeshi ya kikoloni, Mangi Meli alisaidiwa na Jumuiya ya Wakuu wenzake (Njama), wakuu hawa wapo katika picha nyingi za Wajerumani wakiwa na Hans Meyer. Njama walisimama kidete na Mangi Meli katika maisha yake hadi wakati wa kifo chake.
Hii ilitokana na nia yao ya dhati ya kutaka kuipindua serikali ya Kijerumani katika ardhi yao. Mangi Meli pamoja na njama wengine 18 walihukumiwa kifo kama adhabu yao na walinyongwa mbele ya hadhira mnamo Machi 2, 1900 katika mti wa Mgunga ambao upo hadi leo.
Walihukumiwa hapo kwani zamani palikuwa eneo la soko ambalo watu walikuwa wakienda kuuza na kununua bidhaa mbalimbali. Mangi Meli aliona bora afe akitetea eneo lake ambalo Wajerumani chini ya Luteni Merker waliona kama Wachaga hawakuwa na mfumo mzuri.
Mahali alipofanyiwa ukatili panaitwa Tsuduni. Soko hili la Tsuduni lilikuwa karibu na kituo cha jeshi la Wajerumani ambapo waliokuwa wakifika hapo walikuwa wakichunguzwa kiundani na maaskari na wafanyakazi wengine wa jeshi ambao waliwez akuliona soko kutoka kwenye vibaraza vya kituo hicho. Hata sasa kwenye gome la Mgunga, pameendelea kuwa sehemu ya kumbukizi za historia mbalimbali na iliyo muhimu.
Ukatili wa kuwanyonga ulitumika na Wajerumani kama njia ya kudhibiti watu, na ukatili huu ulitekelezwa kwa kutumia njia nyingi miongoni mwa hizo ni mauaji mbele ya hadhira. Matendo kama hayo yalileta hofu ndani ya mioyo ya watu wa jamii husika.
Akizungumza na Kisenaupdate.blogspot.com, Mjukuu wa Mangi anayefahamika Isaria Anael Meli anasema mradi huo waliubuni kutokana na juhudi za zaidi ya miaka kumi ya kutafuta mabaki ya babu yake.
Isaria anasema alikuwa akisimuliwa kuhusu maisha ya babu yake na bibi yake ambaye ni mke mdogo wa Mangi Meli. Katika simulizi hiyo Isaria anasema alijifunza jinsi gani mapambano dhidi ya wakoloni wa Kijerumani nchini Tanzania yalipiganwa chini ya uongozi shupavu wa Mangi Meli kwa ajili ya ukombozi wa watu wake.
Pia Isaria anaongeza kuwa alijifunza jinsi gani mapambano hayo yalisababisha kifo cha babu yake mnamo mwaka 1900 ambapo baada ya kuuawa kichwa cha Mangi Meli kilikatwa na kupelekwa nchini Ujerumani ambako hakijarudi hadi leo.
Licha ya hayo yote mradi huo umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo kubwa kuliko zote ni utashi (uelewa) wa jamii na serikali katika kutunza kumbukumbu zilizobaki za Mangi Meli. Baadhi ya watu wa ukoo wa Mangi Meli wamekuwa wakikosa utashi wa historia yao kwa vizazi vijavyo huku wakiacha vipotee. Jamii nzima ya Old Moshi imekuwa ikichukulia kitu rahisi tu kuacha historia na mabaki ya Mangi wao yapotee.
“Pindi matengenezo yalipoanza ya kuweka kumbukumbu vikwazo vingi vilijitokeza wengi wakidhani tunapiga hela lakini sisi tuliangalia mbele zaidi kwa kizazi kijacho kitafahamu nini kuhusu Mangi Meli mpambanaji,” anasema Isaria.
Pia Halmshauri ya Moshi Vijijini nayo imekuwa ikikosa utashi wa mabaki hayo kwa kuzuia baadhi ya vitu visionyeshwe kwa watalii wanapokuja katika eneo hilo kutaka kujionea kile walichokisoma katika vitabu.
Aidha mdau wa utalii wa utamaduni mkoani Kilimanjaro Gabby Mzei anasema vyombo vya sheria vimekuwa kikwazo katika kuendeleza mradi huo.
“Tulijitolea kusafisha na kupaweka vizuri hapo ilipokuwa mahakama ya Wajerumani, baada ya kuanza kunoga tukapewa barua kuwa hatutakiwa kuwepo hapo na mradi huo haufai kuwepo kwani eneo la mahakama linatakiwa kuwa tulivu na barua tunazo,” anasema Mzei.
Mzei anajiuliza kama kweli serikali ina nia ya dhati ya kutaka utalii wa utamaduni wa asili uhifadhiwe kwani jengo la mahakama lilikuwepo siku nyingi likiliwa na mchwa baada ya kulikarabati ndipo kunaibuka sheria na misimamo isiyokuwa na tija katika uhifadhi.
“Kwani zamani masuala ya mahakama walikuwa wanafanyia wapi? Ni jambo la kushangaza sana; haya basi waturudishie gharama za kulikarabati itapendeza, lakini hilo hatulioni,” anasema Mzei.
Mzei anasema kama serikali ina nia ya dhati ya kupanda kiuchumi lazima wayafanye mabaki ya Mangi Meli kuwa sehemu ya utalii ambao utawaleta wageni wengi nchi ikiwamo kulifuatilia kwa udi na uvumba fuvu la Mangi Meli kama ilivyofanyika kwa Mkwawa wa Uheheni.
Hata hivyo mkazi wa Old Moshi Eliameni Massawe anasema chuki baina ya koo za ndani ya eneo hilo zimekuwa kikwazo cha kufikia malengo ya mradi wa Mabaki ya Mangi Meli kwani ushirikiano katika utoaji wa taarifa na kumbukumbu mbalimbali za Mangi Meli umekuwa mdogo.
Licha ya hayo umuhimu wa hadithi, simulizi kkwenye kuelewa matukio muhimu ya zamani, mke mdogo wa Mangi Meli aliyeitwa Masinde alihakikisha kwamba watu wengi akiwamo mjukuu wake Isaria wanahadithiwa kuhusu ukatili wa mume wake kunyongwa na kuchukuliwa kichwa chake.
MWISHO.





