MOSHI-KILIMANJARO.
KITUO cha Utamaduni na Makumbusho cha Mkoa wa Kilimanjaro kinatarajiwa kuzinduliwa mwezi Julai mwaka huu kwa lengo la kuhifadhi, kuendeleza na kuonesha mila, desturi na urithi wa kihistoria wa wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na mikoa mingine ya Kanda ya Kaskazini.
Hayo yamesemwa Juni 10,2026 na Mhadhiri wa Akiolojia na Turathi kutoka Idara ya Akiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Venance Silayo, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi kuhusu maandalizi ya uzinduzi wa kituo hicho.
Dk. Silayo alisema kituo hicho kitajumuisha maktaba ya urithi, makumbusho ya malikale, utamaduni na utalii, na kitakuwa katika jengo la zamani la Kilimanjaro District Council (KDC), ambalo awali lilitumika kama Baraza la Wachaga.
Alisema kituo hicho kitakuwa kitovu muhimu cha uhifadhi wa historia na utamaduni wa jamii mbalimbali za Kanda ya Kaskazini, huku kikitoa fursa kwa watafiti, wanafunzi na wananchi kupata taarifa na nyaraka mbalimbali zinazohusu urithi wa makabila ya Wachaga, Wapare na Wamasai.
“Tunatarajia kituo hiki kuwa sehemu muhimu ya kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria na kiutamaduni, pamoja na kuchochea tafiti zitakazosaidia vizazi vya sasa na vijavyo kufahamu asili na mila za jamii zetu,” alisema Dk. Silayo.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Beno Chuwa, alisema kabla ya ujio wa dini za kisasa katika maeneo mengi ya Uchagani, wazee wa jadi walikuwa na maeneo maalumu ya ibada na madhabahu walizotumia kuomba dua na baraka kwa ajili ya jamii zao.
Alisema baadhi ya maeneo hayo bado yanatunzwa hadi leo kutokana na umuhimu wake katika historia na utamaduni wa jamii za Wachaga, na kwamba kituo hicho kitasaidia kuyaweka katika kumbukumbu rasmi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye Afisa Utamaduni na Michezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Amoni Sasiel, alisema eneo hilo lina historia kubwa, akieleza kuwa mwaka 1953 majani ya Isale pamoja na miti ya Mracha na Mringaringi vilipandwa kama ishara ya mamlaka na uongozi wa viongozi wa Wachaga waliokuwa wakiongoza maeneo mbalimbali ya Kanda ya Kaskazini.
Alisema eneo hilo pia lilitumika kama sehemu ya shughuli za kijadi na kiutamaduni, jambo linaloonesha umuhimu wa kulihifadhi kama sehemu ya urithi wa taifa.
Uzinduzi wa Kituo cha Utamaduni na Makumbusho cha Mkoa wa Kilimanjaro unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za kuhifadhi historia, mila na desturi za jamii za Kanda ya Kaskazini, sambamba na kukuza utalii wa utamaduni na elimu kwa wananchi.
![]() |








