MOSHI-KILIMANJARO.
ZAIDI ya vijana 160 kutoka kata 16 za Jimbo la Vunjo, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba pamoja na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa yatakayotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wataalamu wengine kutoka Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana.
Hayo yamebainishwa Juni 12,2026, na Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Iddi Mfinanga, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo alisema mafunzo hayo yatakayofanyika Juni 13 mwaka huu katika Kata ya Njiapanda, mji mdogo wa Himo,
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea vijana ujuzi wa kujiajiri kupitia shughuli za ufugaji wa kisasa na ujasiriamali.
Alisema mbali na kupata maarifa ya ufugaji wa samaki, vijana watapatiwa elimu ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa njia za kisasa, ikiwemo namna ya kuchagua mifugo bora, utunzaji wa mifugo, lishe, udhibiti wa magonjwa pamoja na mbinu za kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa manufaa ya kiuchumi.
Mfinanga alisema mafunzo hayo yatafanyika katika Shule ya Msingi Viziwi iliyopo Kata ya Njiapanda, ambapo wataalamu kutoka wizara husika watawawezesha vijana kutambua fursa zilizopo katika sekta ya mifugo na uvuvi na namna ya kuzitumia kujiongezea kipato.
Alifafanua kuwa kati ya vijana watakaoshiriki, 80 watapatiwa mafunzo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba huku wengine 80 wakifundishwa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, hatua inayolenga kuwapa mbadala wa ajira na kuwawezesha kuanzisha miradi yenye tija katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa Mfinanga, mpango wa kuwashirikisha vijana katika shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji unalenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi sambamba na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha ulaji wa samaki nchini bado ni wastani wa kilo 7.9 kwa mtu kwa mwaka, kiwango ambacho kiko chini ya wastani wa kilo 20 zinazopendekezwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), hali inayoonesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika miradi ya ufugaji wa samaki ili kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko.
“Vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa na wana nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya uchumi ikiwa watapatiwa ujuzi na fursa sahihi. Mafunzo haya yatawawezesha kuanzisha na kuendesha shughuli za ufugaji wa samaki kwa vizimba, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na miradi mingine ya mifugo kwa njia ya kibiashara,” alisema.
Serikali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali imeendelea kuwekeza katika utoaji wa mafunzo ya stadi za ufugaji na kilimo biashara kwa vijana, ikiwa ni mkakati wa kukuza ajira, kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha ya wananchi.
![]() |








