KILIMANJARO PLANTATION FC YATINGA ROBO FAINALI, YAIONDOA NJORO UNITED KWA MIKWAJU YA PENALTI


 MOSHI-KILIMANJARO 

TIMU ya Kilimanjaro Plantation FC imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Zuberi Cup, baada ya kuiondoa Njoro United FC kwa ushindi wa mabao 5-4 kwa mikwaju ya penalti, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo.

Mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Railway uliopo Kata ya Njoro ulikuwa na ushindani mkubwa, huku kila timu ikionyesha nidhamu na umakini mkubwa katika kupanga mashambulizi na kujilinda, kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare ya 0-0 baada ya pande zote kushindwa kutumia nafasi walizozipata.

Kipindi cha pili kilishuhudia Kilimanjaro Plantation FC ikiongeza kasi ya mashambulizi na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, lakini washambuliaji wake walikosa umakini wa kuzitumia.

Njoro United FC nao walipata nafasi za kusaka bao la ushindi, lakini walishindwa kuzitumia na hivyo kufanya mchezo kumalizika kwa sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90.

Katika mikwaju ya penalti, Kilimanjaro Plantation FC walionyesha utulivu na umakini mkubwa kwa kushinda mabao 5-4, ushindi uliowapa tiketi ya kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Kufuatia ushindi huo, Kilimanjaro Plantation FC imeungana na timu za Green Eagle FC, Kibo Warriors FC, Mandela Rangers FC, Kilimanjaro Wonders FC na Lafamilia FC, ambazo tayari zimejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali ya Zuberi Cup.

Hadi sasa, timu sita zimefuzu hatua ya robo fainali, huku nafasi mbili zilizobaki zikitarajiwa kuamuliwa katika michezo iliyosalia ya hatua ya 16 bora.

Mashindano ya Zuberi Cup yanaendelea kuvutia mashabiki wengi kutokana na ushindani mkubwa na nafasi yake ya kuibua vipaji vya soka katika Mkoa wa Kilimanjaro.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.