KAMATI ZA USHAURI WA KISHERIA ZAIWEZESHA KILIMANJARO KUNG'ARA KITAIFA

MOSHI-KILIMANJARO.

KUANZISHWA kwa Kamati za Ushauri wa Kisheria chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kumeendelea kuleta matokeo chanya katika kuimarisha utawala wa sheria, utatuzi wa migogoro na upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi, huku Mkoa wa Kilimanjaro ukitajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika utekelezaji wa mfumo huo.

Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Kilimanjaro, Tamari Mdeme, alisema mafanikio hayo yameiwezesha Mkoa wa Kilimanjaro kutunukiwa tuzo maalum kutokana na ushirikiano mkubwa unaotolewa na uongozi wa mkoa katika kuimarisha utawala bora wa kisheria na kuboresha upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Alisema kupitia Kamati za Ushauri wa Kisheria, mkoa umeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kuimarisha uwajibikaji, kuharakisha utatuzi wa migogoro kwa kuzingatia sheria na kuweka msingi wa suluhisho la kudumu kwa kero za wananchi, hatua inayochangia kuimarisha utawala wa sheria katika Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro, Jones Mola, alisema migogoro ya ardhi imeendelea kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili wananchi, sambamba na kuvunjika kwa ndoa na migogoro ya kifamilia ambayo imechangia kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Askofu Mola aliipongeza Serikali kwa kuanzisha Kamati za Ushauri wa Kisheria, akisema zimekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza migogoro hiyo kwa kutoa ushauri wa kisheria, kuhamasisha maridhiano na kusaidia wananchi kutatua migogoro yao kwa njia ya amani na kwa kuzingatia sheria.

Kutokana na mafanikio hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alipokea tuzo maalum kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutambua mchango wa mkoa katika kuimarisha utawala wa sheria, utoaji wa haki na ushirikiano na taasisi za kisheria.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo ofisini kwake, Babu aliishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutambua juhudi zinazofanywa na Mkoa wa Kilimanjaro, akisema tuzo hiyo ni heshima kwa wananchi wa mkoa huo na motisha wa kuendelea kusimamia misingi ya utawala bora pamoja na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Aidha, alisema Mkoa wa Kilimanjaro utaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi zote za kisheria ili kuimarisha utoaji wa huduma za haki, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya sheria na kujenga jamii inayozingatia misingi ya utawala wa sheria.

Mkoa wa Kilimanjaro umeendelea kujijengea sifa katika sekta mbalimbali kutokana na uongozi thabiti, uwajibikaji na ushirikiano unaotekelezwa na viongozi wake katika kuhudumia wananchi, hali iliyochangia kutambuliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia tuzo hiyo maalum.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.