WANANCHI 42,283 KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI MOSHI

MOSHI-KILIMANJARO.

WANANCHI 42,283 kutoka katika kata za Kaloleni, Njoro na Miembeni, Manispaa ya Moshi, wanatarajiwa kunufaika na mradi wa upanuzi wa chanzo cha maji cha Coffee Curing, unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA).

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa MUWSA, Mhandisi Brayson Saria, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa chanzo hicho mbele ya Kamati ya Siasa ya CCM ya Moshi Mjini.

Alisema lengo la mradi huo ni kuongeza uzalishaji wa maji na kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama katika Manispaa ya Moshi, hususan katika kata hizo tatu zenye jumla ya wakazi 42,283.

Kwa mujibu wa Mhandisi Saria, mradi huo unatarajiwa kugharimu jumla ya Sh milioni 646.1, ambapo awamu ya kwanza imegharimu Sh milioni 70, huku awamu ya pili ikigharimu Sh milioni 576.1.

Alisema utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo tayari umekamilika kwa asilimia 100, huku awamu ya pili ikitarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu na kukamilika Juni 2027.

Alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia wananchi wa Manispaa ya Moshi na maeneo mengine kupata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika na kwa njia endelevu.

“Wakati wa utekelezaji wa mradi, ajira za moja kwa moja zimetolewa kwa vijana, pamoja na ajira zisizo rasmi kwa wanawake, hasa akina mama lishe ambao wamekuwa wakijishughulisha na upishi wa chakula kwa ajili ya mafundi,” alisema.

Aidha, alisema MUWSA kwa sasa inazalisha jumla ya mita za ujazo 43,322 za maji kwa siku, sawa na asilimia 60 ya mahitaji ya Manispaa ya Moshi ambayo ni mita za ujazo 73,246 kwa siku.

Alisema Manispaa ya Moshi inakabiliwa na upungufu wa maji wa takribani mita za ujazo 17,593 kwa siku, hali iliyosababisha mamlaka hiyo kuanza kutekeleza mradi wa upanuzi wa chanzo cha Coffee Curing.

Alifafanua kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo, uzalishaji wa maji katika chanzo cha Coffee Curing utaongezeka kutoka mita za ujazo 750 hadi kufikia mita za ujazo 3,840 kwa siku.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.