MOSHI-KILIMANJARO.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, amepongeza utendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA), kwa juhudi zake za kuboresha huduma na kutekeleza miradi ya kimkakati ya upatikanaji wa majisafi na salama katika maeneo mbalimbali.
Makoi alitoa pongezi hizo jana, wakati wa uzinduzi wa vifaa vya mradi wa uboreshaji wa miundombinu chakavu ya majisafi katika Kata ya Uru Mashariki, Wilaya ya Moshi, akisema MUWSA imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.
Alisema pamoja na MUWSA kuhudumia maeneo mengi, imeendelea kuipa kipaumbele Jimbo la Moshi Vijijini kwa kutekeleza miradi inayolenga kutatua changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali.
![]() |
Akizungumzia mradi wa uboreshaji wa miundombinu chakavu ya majisafi katika Kata ya Uru Mashariki, Makoi amesema eneo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu, huku kijiji cha Materuni kikiwa ni miongoni mwa vijiji vya mwisho vilivyopo katika maeneo ya mlima.
Alisema tatizo hilo lilikuwa likivihusu vijiji vya Materuni, Mwasi Kusini, Mnini, Kyaseni, Mwasi Kaskazini, Mruwia na Kishimundu, ambavyo kwa muda mrefu vilikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi.
“Tatizo la maji lilikuwa kubwa katika vijiji hivi, namshukuru Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kwa kunipatia mabomba ya maji yaliyogharimu Sh milioni 170 kwa ajili ya kusaidia kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika kata hii,” alisema.
Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa kazi ya uboreshaji wa mtandao chakavu wa majisafi katika Kata ya Uru Mashariki, Msimamizi wa Mradi kutoka MUWSA, Ally Lukwarо, alisema mradi huo unatarajiwa kunufaisha wakazi 14,179 wa vijiji saba vilivyopo katika kata hiyo.
Kwa mujibu wa Lukwarо, utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu na kukamilika Desemba mwaka huu, ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na uchimbaji wa mtaro kwa ajili ya ulazaji wa mabomba.
"Mradi huo utagharimu Sh milioni 170.6 hadi kukamilika kwake na unatarajiwa kuwafikia wakazi wapatao 14,179 wa kata hiyo.
![]() |
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza adha kubwa iliyokuwa ikiwakabili wananchi ambao walilazimika kutafuta huduma ya maji katika maeneo ya mbali.
"Mradi huo ni muhimu kwa wananchi wa kata hii kwa kuwa utaongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama na kupunguza muda na gharama ambazo wananchi wamekuwa wakitumia kutafuta maji."alisema.






















