MOSHI-KILIMANJARO.
UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Moshi Mjini, unatarajia kuadhimisha Wiki ya UWT kwa kutembelea kituo kinachotoa huduma kwa watoto wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali za kijamii zitakazofanyika Oktoba Mosi, mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Katibu wa UWT Wilaya ya Moshi Mjini, Catherine Sarwatt, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuelekea maadhimisho hayo yanayofanyika kesho, Oktoba Mosi, mwaka huu.
Sarwatt alisema katika maadhimisho hayo, UWT imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kutembelea maeneo yanayotoa huduma kwa makundi yenye mahitaji maalumu, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mwenyekiti wa Taifa wa UWT.
![]() |
“Katika Wiki ya Maadhimisho ya UWT Wilaya ya Moshi Mjini, Oktoba Mosi tutakwenda Shule ya Msingi Shirimatunda, kitengo cha watoto wenye ulemavu wa akili, kwa ajili ya kuwapatia msaada wa kijamii,” alisema Sarwatt.
Aidha, alisema baada ya kutembelea kituo hicho, UWT itaelekea katika ofisi za CCM za kata ya Shirimatunda ambako utafanyika mkutano wa wanachama na wananchi kwa ajili ya kusikiliza na kujadili kero zinazowakabili.
Alisema mkutano huo pia utatumika kuwashukuru wananchi kwa ushiriki wao katika Uchaguzi mkuu wa Rais, Waabunge na Madiowani wa mwaka 2025, pamoja na kutoa elimu kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi cha msimu wa Vuli.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Moshi Mjini na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya, Theresia Komba, anatarajiwa kuhutubia wananchi hao.
Sarwatt alisema pia Afisa Mazingira atatoa elimu kuhusu maandalizi na tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likitoa elimu ya namna ya kukabiliana na majanga na kuchukua hatua za usalama wakati wa mvua.
Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii atatoa elimu kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi mbalimbali kupitia Mamlaka za serikali za Mitaa, pamoja na namna wananchi wanavyoweza kunufaika na fursa hiyo.






