MOSHI-KILIMANJAR..
MSANII wa ngoma za asili na Mwenyekiti wa Kikundi cha Ngoma za Msanja, kilichopo Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi, Biusi Kipingu, amesema tasnia ya sanaa mkoani Kilimanjaro inakabiliwa na changamoto mbalimbali, hali inayowafanya wasanii wengi kushindwa kuendeleza vipaji vyao.
Kipingu amesema pamoja na kuwepo kwa wasanii wengi wenye vipaji mkoani humo, baadhi yao wanashindwa kufikia malengo yao kutokana na mazingira magumu ya kifedha pamoja na ukosefu wa watu wa kuwaongoza na kuwapa miongozo sahihi katika safari yao ya kisanaa.
Akizungumza wakati wa Usiku wa Msanja na MC Biusi, amesema changamoto hizo zimekuwa zikikwamisha wasanii wenye vipaji kufikia hatua ya kutambulika ndani na nje ya Tanzania.
![]() |
Amesema ili kukuza na kuendeleza vipaji vya wasanii mkoani Kilimanjaro, kuna umuhimu wa wadau mbalimbali wa sanaa, taasisi na Serikali kuweka mazingira yatakayowasaidia wasanii kupata elimu, miongozo na fursa za kifedha kwa ajili ya kuendeleza kazi zao.
Kikundi cha Ngoma za Asili cha Msanja kilianzishwa mwaka 1990, kikiwa na maono ya kutumia sanaa kama nyenzo ya kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii.
Kikundi hicho kimeendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za sanaa, huku kikilenga kuendeleza na kuhifadhi utamaduni kupitia ngoma za asili.













