Mdhamini wa mashindano ya Zuberi Cup Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, (kulia), akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava.
MOSHI-KILIMANJARO
KADRI mashindano ya Zuberi Cup yanavyozidi kusonga mbele, ndivyo yanavyoendelea kuthibitisha kuwa si mashindano ya kawaida ya soka la jamii, bali ni jukwaa muhimu la kukuza vipaji, kuimarisha ushindani na kutoa fursa kwa vijana wengi kutimiza ndoto zao za kucheza soka la kulipwa.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021, mashindano hayo yameendelea kuvutia mamia ya wachezaji na maelfu ya mashabiki kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro, huku kila msimu ukionyesha kiwango kikubwa zaidi cha ushindani.
Msimu huu wa Zuberi Cup umeendelea kuandika historia nyingine baada ya timu ya Kilimanjaro Plantation FC kufuzu hatua ya robo fainali kwa ushindi wa mabao 5-4 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Njoro United FC.
Ushindi huo ulipatikana baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Railway uliopo Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi.
Mchezo huo ulikuwa wa kuvutia na wenye ushindani mkubwa kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, timu zote mbili ziliingia uwanjani zikiwa na lengo la kusonga mbele, jambo lililozifanya kucheza kwa nidhamu kubwa huku kila upande ukijikita zaidi katika kujilinda na kusaka ushindi.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare ya bila kufungana, licha ya kila timu kupata nafasi chache za kutikisa nyavu, baada ya mapumziko, Kilimanjaro Plantation FC waliongeza kasi ya mchezo na kuonyesha dhamira ya kutafuta bao la ushindi.
Walitengeneza nafasi kadhaa nzuri, lakini washambuliaji wao walikosa utulivu na kushindwa kuzitumia ipasavyo. Njoro United FC nao walijibu kwa mashambulizi ya kushtukiza yaliyowapa matumaini ya kupata bao, lakini walikumbana na safu imara ya ulinzi wa wapinzani wao pamoja na ukosefu wa umakini katika umaliziaji.
Kutokana na sare hiyo, mshindi aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti, Kilimanjaro Plantation FC walionyesha utulivu mkubwa na kutumia vizuri nafasi zao, wakishinda kwa mabao 5-4 na kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali.
Ushindi huo uliibua shangwe kubwa kwa mashabiki wao waliokuwa wamejitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo, kwa matokeo hayo, Kilimanjaro Plantation FC imeungana na Green Eagle FC, Kibo Warriors FC, Mandela Rangers FC, Kilimanjaro Wonders FC na Lafamilia FC ambazo tayari zilikuwa zimefuzu hatua ya robo fainali.
Kufikia sasa timu sita zimekata tiketi ya hatua hiyo, huku nafasi mbili zilizobaki zikisubiri kuamuliwa katika michezo iliyobaki ya hatua ya 16 bora.
Mwenyekiti wa mashindano ya Zuberi Cup, Mwalimu Japheti Mpande, amesema msimu huu umeshirikisha jumla ya timu 38 kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema baada ya kumalizika kwa hatua ya awali, timu 16 zilifuzu hatua ya 16 bora na sasa ushindani umehamia robo fainali, hatua ambayo inatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa kutokana na ubora wa timu zilizobaki.
Kwa mujibu wa Mpande, mafanikio ya mashindano hayo yanatokana na ushirikiano mkubwa kati ya waandaaji, wadhamini, viongozi wa soka, mashabiki na jamii kwa ujumla.
Amesema kila mwaka mashindano hayo yanaendelea kukua na kuwa kivutio kikubwa kwa vijana wanaotaka kuonyesha uwezo wao mbele ya wasaka vipaji kutoka klabu mbalimbali nchini.
Naye mdhamini wa mashindano hayo, ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, amesema Zuberi Cup imekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya soka la mkoa huo.
Amesema tangu mashindano hayo yaanze mwaka 2021, vijana wengi waliokuwa wakicheza katika viwanja vya mitaani wamepata nafasi ya kuonekana na kusajiliwa na klabu zinazoshiriki ligi mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Kidumo, mafanikio hayo yanaonekana kupitia wachezaji waliofanikiwa kupanda ngazi za soka kutokana na mashindano hayo. Miongoni mwao ni Selemani Mwalimu, anayemilikiwa na Wydad Casablanca na ambaye kwa sasa anaitumikia Simba SC kwa mkopo.
Wengine ni Daniel Lyanga, Selemani Bwenzi wa Mshujaa FC na Ramadhan Chobwedo wa TRA United, huku wachezaji wengine wengi wakiendelea kufuatiliwa na wasaka vipaji.
Mbali na kuibua vipaji, Zuberi Cup imekuwa kichocheo cha shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka viwanja vinavyotumika kwa michezo hiyo. Kila mechi huvutia mamia ya mashabiki wanaonunua bidhaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara wadogo, mama lishe, bodaboda na wauzaji mbalimbali, hali inayochangia kuongeza kipato kwa wananchi.
Wadau wa michezo wanaamini kuwa mashindano hayo yamekuwa mfano bora wa namna soka la jamii linavyoweza kutumika kuunganisha watu, kukuza vipaji na kuibua fursa za ajira kwa vijana.
Aidha, uwepo wa wasaka vipaji katika baadhi ya mechi unawapa hamasa wachezaji kujituma zaidi wakiamini kuwa kila mchezo unaweza kubadilisha maisha yao.
Kadri mashindano yanavyoelekea hatua za mwisho, ushindani unazidi kuwa mkubwa na kila timu inaingia uwanjani ikiwa na ndoto ya kutwaa ubingwa, hata hivyo, jambo kubwa zaidi linalobaki kuwa urithi wa Zuberi Cup ni mafanikio yake katika kuibua vipaji, kuimarisha uchumi wa wananchi na kuifanya Kilimanjaro kuwa moja ya maeneo yanayoendelea kuzalisha wachezaji wenye uwezo wa kucheza soka la ushindani ndani na nje ya Tanzania.









