VUNJO-MOSHI
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, amekabidhi vifaa vya michezo kwa timu 16 zinazoshiriki mashindano ya Koola Vunjo Cup 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono vijana na kukuza vipaji vya soka katika Jimbo la Vunjo.
Makabidhiano ya vifaa hivyo yalifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mashindano hayo uliofanyika katika Uwanja wa Polisi Himo.
Mashindano hayo yanashirikisha timu 16 kutoka katika kata 16 zinazounda Jimbo la Vunjo, ambapo kila kata imewakilishwa na timu moja.
Koola Vunjo Cup imeanzishwa na Mbunge Enock Zadock Koola, kwa lengo la kutoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao, kuviendeleza na kuwaandaa kwa hatua za juu zaidi za ushindani katika soka.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, Koola amesema michezo, hususan mpira wa miguu, inaweza kuwa fursa muhimu kwa vijana kujenga maisha yao endapo watazingatia nidhamu, kujituma na kutumia vipaji walivyonavyo.
Katika mchango huo, kila timu imekabidhiwa seti mbili za jezi pamoja na mipira miwili kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Moshi, Morris Makoi, amewataka vijana wanaoshiriki mashindano hayo kutumia fursa hiyo kuonyesha vipaji na talanta walizonazo, huku wakiongeza bidii, juhudi na nidhamu ili kufikia malengo yao katika soka.
Makoi amempongeza Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuendeleza michezo, akisema mashindano hayo ni sehemu ya jukwaa la kuwapa vijana fursa ya kuonyesha uwezo wao, kuibua vipaji vipya na kuwaandaa wachezaji ambao wanaweza kuwakilisha Vunjo, Kilimanjaro na Taifa katika hatua za juu za soka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amempongeza Mbunge Koola kwa kuanzisha mashindano hayo na kuwekeza katika kukuza vipaji vya vijana.
Mnzava amesema mashindano hayo yana umuhimu mkubwa katika kuibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi, ambao baadaye wanaweza kuwa sehemu ya hazina ya soka katika Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla.
“Nikupongeze kwa moyo wako wa uzalendo. Sio kwamba una fedha nyingi sana, lakini kile kidogo unachokipata umeona ushirikiane na watu wako wa Jimbo la Vunjo,” amesema Mnzava.
Akizungumzia muundo wa mashindano hayo, Mwenyekiti wa mashindano ya ligi ya Koola Vunjo Cup, Japhari Agustino Kalinga, amesema michezo hiyo itafanyika katika viwanja vinne, ambavyo vitatumika kwa ajili ya kuendesha ratiba ya mashindano.
Ametaja viwanja hivyo kuwa ni Chuo cha Ualimu TTC Marangu, Uchira, Polisi Himo na Mandaka.
Kalinga amesema kila uwanja utahusisha timu nne kutoka katika maeneo mbalimbali, huku michezo ikiendelea kwa awamu hadi kupatikana timu zitakazofuzu hatua zinazofuata za mashindano.
Katika mchezo wa ufunguzi, timu kutoka Kata ya Makuyuni itakutana na timu kutoka Kata ya Njia Panda Himo, katika mchezo unaotarajiwa kuashiria mwanzo rasmi wa safari ya Koola Vunjo Cup 2026.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa vijana wa Jimbo la Vunjo kuonyesha uwezo wao, huku wadau wa michezo wakitarajiwa kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha vipaji vinavyobainika vinapata nafasi ya kuendelezwa.



















