USHINDI WA HAI UNITED WAAPA KUNYAKUA UBINGWA ZUBERI CUP

MOSHI-KILIMANJARO.

TIMU ya Hai United imeapa kupambana kwa nguvu zote katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Zuberi Cup, ikilenga kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki.

Hai United imefuzu hatua ya robo fainali baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bondeni FC katika mchezo wa mwisho wa hatua ya 16 bora, uliochezwa kwa ushindani mkubwa na kushuhudia timu zote zikifanya mashambulizi ya kutafuta ushindi.

Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Amani Balinoti dakika ya 87, baada ya Hai United kutumia vizuri nafasi iliyopatikana katika dakika za mwisho za mchezo na hivyo kufunga safari ya kuelekea hatua ya robo fainali.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Hai United, Shaban Msango, alisema ushindi huo umeongeza ari kwa wachezaji wake na kuwapa nguvu zaidi ya kujiandaa kwa ajili ya hatua inayofuata.

Msango alisema lengo lao si kufika robo fainali pekee, bali kuhakikisha wanapambana kwa nguvu zote ili kufikia hatua ya mwisho na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

“Ushindi huu tulio upata unatupa ari zaidi ya kupambana kufa na kupona katika robo fainali. Tunaenda kujiandaa kwa ajili ya mechi zinazofuata na niwahakikishie mashabiki wetu hatutawaangusha. Zawadi pekee kwetu ni kuwapa ushindi,” alisema Msango.

Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Bondeni FC, Peter Majogoro, alisema vijana wake walicheza vizuri na kuonyesha uwezo mkubwa, lakini walishindwa kutumia nafasi walizopata, hasa katika dakika za mwisho za mchezo.

Majogoro alisema hali hiyo iliwapa nafasi wapinzani wao kutumia mapungufu yaliyokuwepo na kupata bao lililowafanya Bondeni FC kuondolewa kwenye mashindano.

“Vijana walicheza vizuri na kuonyesha uwezo wao mzuri wa kucheza, japokuwa tulishindwa kumalizia mchezo katika dakika za mwisho na wapinzani wetu wakatumia mapungufu hayo kutuadhibu,” alisema Majogoro.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, ameipongeza Hai United kwa ushindi huo na kufuzu hatua ya robo fainali, akisema timu hiyo imeonyesha kuwa ina uwezo wa kwenda mbali katika mashindano hayo.

Bomboko alisema Hai United tayari ni mabingwa wa Mkoa na imewahi kufanya vizuri katika hatua ya Kanda, hivyo matarajio yao sasa ni kuona timu hiyo ikiandika historia kwa kutwaa ubingwa wa Zuberi Cup katika ushiriki wao wa kwanza.

“Hai United ndiyo mabingwa wa Mkoa na sisi tulifanikiwa kwenda Kanda. Tunao wachezaji wazuri, matarajio yetu ni kuwa mabingwa wa mashindano ya Zuberi Cup. Kwa mara ya kwanza tumeshiriki mashindano haya na kwa mara ya kwanza tunakwenda kuchukua kombe hili,” alisema Bomboko.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alimshukuru mdhamini wa mashindano hayo kwa kuendelea kuyaendesha na kuyawezesha, akisema Zuberi Cup imekuwa jukwaa muhimu kwa vijana kupata fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kujenga uwezo kupitia soka.

Bomboko pia alitumia nafasi hiyo kuipa Hai United changamoto kuelekea robo fainali, akitaka wachezaji kuongeza umakini na kupambana kwa nguvu ili kuhakikisha wanaendelea na safari ya kuwania ubingwa.

Katika mchezo huo dhidi ya Bondeni FC, mashambulizi yalikuwa yakitoka pande zote mbili, huku kila timu ikitafuta nafasi ya kupata bao la kuongoza. Hata hivyo, uimara wa safu za ulinzi uliifanya mechi hiyo kuendelea bila bao hadi dakika za mwisho.

Hai United ilifanikiwa kutumia nafasi hiyo dakika ya 87 kupitia Balinoti, aliyefunga bao lililoleta shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo na kuiwezesha kufuzu robo fainali kwa ushindi wa bao 1-0.

Naye Diwani wa Kata ya Bondeni, Haji Fandi, alisema licha ya timu yake kucheza vizuri na kuonyesha kiwango cha kuridhisha, wapinzani wao walifanikiwa kutumia mapungufu madogo yaliyotokea na kuwaadhibu.

Kwa ushindi huo, Hai United sasa inaweka nguvu zake katika maandalizi ya robo fainali, huku ikibeba matumaini ya mashabiki wa Hai ambao wanaamini timu hiyo inaweza kufanya vizuri zaidi na hatimaye kutwaa kombe hilo.

Safari ya Hai United kuelekea ubingwa sasa inaingia katika hatua muhimu, ambapo kila mchezo utahitaji maandalizi, nidhamu na umakini mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuzuia makosa yaliyoweza kuigharimu timu katika hatua zilizopita.

Kwa upande wa mashabiki, ushindi wa dakika za mwisho dhidi ya Bondeni FC umeongeza matumaini kwamba timu hiyo inaweza kuendelea kufanya vizuri na kutimiza azma ya kuandika historia mpya katika mashindano ya Zuberi Cup.















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.