WANANCHI KISANGARA WAIPONGEZA TAKUKURU KUREJESHA PIKIPIKI YA KIJIJI


MWANGA-KILIMANJARO.

WANANCHI wa Kijiji cha Kisangara, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, wameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kufanikisha kurejeshwa kwa pikipiki ya ofisi ya kijiji hicho iliyokuwa imesajiliwa kwa jina binafsi la aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji, Brayson Laurent Msofe.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa kwa pikipiki hiyo, wananchi hao wamesema elimu ya mapambano dhidi ya rushwa inayotolewa na TAKUKURU imeongeza uelewa na kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma. Mkazi wa kijiji hicho, John Elias, amesema wananchi wanaishukuru TAKUKURU kwa kusimamia haki na kuhakikisha mali ya kijiji inarejeshwa ili kuendelea kutumika katika kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalum Kata ya Kisangara, Neophita Mlacha, pamoja na Mtendaji wa Kata hiyo, Glory Maelezo, walisema kurejeshwa kwa pikipiki hiyo kutasaidia utekelezaji wa shughuli za maendeleo ikiwemo ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma kwa wananchi.

 Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisangara, Halima Mdee, alisema tukio hilo ni fundisho kwa viongozi wote wanaopewa dhamana ya kusimamia mali za umma, akisisitiza umuhimu wa kuzitunza na kuzitumia kwa manufaa ya wananchi.

 Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hiyo, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Sabas Salehe Mmbaga, amesema uchunguzi wa taasisi hiyo ulibaini kuwa fedha za kununua pikipiki hiyo zilitolewa mwaka 2025 kwa ajili ya matumizi ya kijiji, lakini mali hiyo ilisajiliwa kwa jina binafsi badala ya kijiji.

Amesema baada ya kufuatiliwa na TAKUKURU, mhusika alikiri makosa yake na kununua pikipiki nyingine iliyorejeshwa kwa kijiji. Aidha, TAKUKURU imetoa wito kwa viongozi wote wanaosimamia mali za umma kuhakikisha zinatumika kwa manufaa ya wananchi na si kwa maslahi binafsi.


Aidha, TAKUKURU imetoa wito kwa viongozi wote wanaosimamia mali za umma kuhakikisha mali hizo zinatumika kwa manufaa ya wananchi na si kwa maslahi binafsi, ikisisitiza kuwa kufanya kinyume chake ni ukiukwaji wa maadili na sheria za utumishi wa umma.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.