VIJANA 300 KUTOKA JIMBO LA VUNJO WANOLEWA UFUGAJI WA SAMAKI, NG'OMBE WA MAZIWA

VUNJO-KILIMANJARO 

ZAIDI ya vijana 300 kkutokaJimbo la Vunjo, Halmashauri  ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamepatiwa mafunzo ya ufugaji wa samaki na ng’ombe wa maziwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri, kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato kupitia Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Mafunzo hayo yaliyofanyika jana katika Shule ya Viziwi Njiapanda, mji mdogo wa Himo, yaliandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, kwa lengo la kuwajengea uwezo wananchi katika sekta za Mifugo na Uvuvi ili kukuza uchumi wa kaya.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkufunzi Mwandamizi kutoka Wakala wa Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Tengeru (LITA), Iman Sichalwe, aliwataka wafugaji kuachana na ufugaji wa mazoea na badala yake kuzingatia ushauri wa wataalamu ili kuongeza tija na ubora wa mifugo yao.

Alisema matumizi ya mbinu za kisasa za ufugaji, lishe bora na huduma za afya ya mifugo vinaweza kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuboresha afya ya mifugo na kuongeza mapato ya wafugaji kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi, Mariam Hamisi Chupasa, aliwapatia washiriki elimu kuhusu ufugaji wa samaki aina ya Sato na Kambale, utengenezaji wa chakula cha samaki pamoja na ujenzi na usimamizi wa mabwawa na vizimba vya kufugia samaki.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Katibu wa Mbunge huyo, Iddy Mfinanga, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha wananchi kujiajiri na kutumia fursa zilizopo katika sekta za mifugo na uvuvi ili kuboresha maisha yao.

Mfinanga alisema Mbunge Koola anaendelea kuwekeza katika elimu na mafunzo ya uzalishaji mali kwa wananchi wake kwa kuwa anaamini maarifa ni nyenzo muhimu ya kupambana na umaskini na kuongeza maendeleo ya jamii.

Baadhi ya washiriki walimshukuru Mbunge Koola kwa kuwaandalia mafunzo hayo, wakisema yamewapa ujuzi wa kutengeneza chakula cha mifugo aina ya silage na mbinu bora za ufugaji ambazo zitawawezesha kuongeza uzalishaji na kipato katika shughuli zao za kila siku.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.