MWANGA-KILIMANJARO.
MBUNGE wa Jimbo la Mwanga, Dk. Ngwaru Maghembe, amesema ataendelea kushughulikia na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo kadri rasilimali na fedha za maendeleo zinavyopatikana.
Dk. Maghembe alitoa kauli hiyo Juni 13,2026 wakati wa ziara yake ya kuwashukuru wananchi na kusikiliza kero zao katika kata za Shighatini, Msangeni na Mwanga, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kutembelea kata zote 20 za jimbo hilo.
Akiwa katika Kijiji cha Mfinga, Kata ya Shighatini, alipokea malalamiko kuhusu uchakavu wa miundombinu ya shule, uhaba wa vyoo, changamoto ya maji safi na salama, ubovu wa barabara pamoja na upungufu wa madarasa katika baadhi ya shule.
Katika Kata ya Msangeni, Tarafa ya Ugweno, wananchi walieleza changamoto za ukosefu wa bima ya afya kwa wazee, maji safi na salama, uchakavu wa miundombinu ya elimu pamoja na hali mbaya ya baadhi ya barabara za kata hiyo. Aidha, katika Kata ya Mwanga wananchi waliwasilisha kero zinazohusu maji, barabara, huduma za bima ya afya na uchakavu wa miundombinu ya soko.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Dk. Maghembe aliwashukuru wananchi kwa imani waliyoonyesha kwake katika uchaguzi mkuu uliopita na kuwawezesha kuwa mwakilishi wao bungeni, huku akiahidi kuendelea kutafuta fedha za miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
"Hata kama hamnioni jimboni mara kwa mara, ninaendelea kutekeleza majukumu yenu nikiwa bungeni. Kazi yangu kubwa ni kutafuta fedha za maendeleo na kusimamia utekelezaji wa miradi inayowanufaisha wananchi. Tayari zaidi ya walimu 65 wameletwa wilayani hapa ili kuboresha sekta ya elimu," alisema Dk. Maghembe.
Dk. Maghembe, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, imeanza kutekeleza ahadi mbalimbali kwa wananchi wa Mwanga, ikiwemo kupeleka magari mawili ya zimamoto, boti ya uokozi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na fedha za miradi ya elimu.
Alisema zaidi ya Sh milioni 170 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika shule za Katola na Kivisini, fedha za ujenzi wa vyoo katika Shule ya Sekondari Vudoe pamoja na zaidi ya Sh milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Wasichana Asharose Migiro iliyoharibiwa na moto.
Hadi sasa, Dk. Maghembe ameshatembelea kata 18 kati ya 20 za Jimbo la Mwanga, huku kata za Kifula na Mwaniko zikiwa bado kufikiwa katika mwendelezo wa ziara hiyo.











