MOSHI-KILIMANJARO.
KATIBU Tawala Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Kiseo Nzowa, ameushauri uongozi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira na kuhifadhi vyanzo vya maji ili kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu inakuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ushauri huo ulitolewa Juni 18,2026 alipokutana na Wajumbe wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani pamoja na Menejimenti ya taasisi hiyo ofisini kwake, wakati wa majadiliano kuhusu utekelezaji wa mradi wa Mto Kikuletwa unaolenga kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo mafuriko yanayosababishwa na mto huo kufurika wakati wa msimu wa mvua.
Alisema bado kuna changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji, katika baadhi ya maeneo kutokana na shughuli za kibinadamu, hususan ukataji miti na uvamizi wa maeneo ya vyanzo vya maji, hali inayohitaji kupewa kipaumbele kupitia utoaji wa elimu na usimamizi wa Sheria za mazingira.
Aidha, aliwashauri Wajumbe wa Bodi hiyo kuhamasisha matumizi ya mita za maji za kulipia kabla ya matumizi (Prepaid Meters) ili kupunguza tatizo la madeni ya maji, hasa kwa taasisi mbalimbali, jambo ambalo alisema limekuwa likikwamisha utoaji wa huduma bora katika sekta ya maji.
Alisema upatikanaji wa mapato ya uhakika kupitia mfumo huo utawezesha Mamlaka za Maji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, huku ukisaidia kudhibiti upotevu wa maji na kuimarisha usimamizi wa huduma za maji nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PBWB, Mhandisi Ruth KoyaKoya, aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kuendelea kutoa ushirikiano unaowezesha PBWB kuendelea kutekeleza majukumu yake ya usimamizi wa rasilimali za maji.
Naye Mkurugenzi wa PBWB, Mhandisi Segule Segule, alisema mradi huo unatekelezwa katika Mto Kikuletwa uliopo mpakani mwa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Aidha alisema kuwa mvua kubwa zilizonyesha mwanzoni mwa miaka ya 2000 zilisababisha mto huo kupanuka na kuunda mkondo mpya, ambapo sehemu kubwa ya maji iliingia katika makazi na mashamba ya wananchi na kusababisha uharibifu mkubwa.
Mhandisi Segule alisema kazi inayoendelea sasa ni kusafisha na kurejesha mkondo wa mto huo katika njia yake ya asili, ili kupunguza hatari ya mafuriko na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi.










