DIWANI KATA YA SHINGHATINI AIOMBA SERIKALI KUHARAKISHA UTATUZI WA CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI KATA HIYO

SHIGHATINI-MWANGA.

DIWANI wa Kata ya Shighatini, Joseph Mrutu, ameiomba Serikali kuharakisha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili kata hiyo, zikiwemo uchakavu wa miundombinu ya shule, upungufu wa vyoo, huduma za afya, maji safi na salama pamoja na ubovu wa barabara.

Mrutu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, alieleza changamoto hizo wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Dk. Ngwaru Maghembe, ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kata hiyo.

Alisema Kata ya Shighatini ina shule sita za msingi za serikali ambazo kwa sasa zinakabiliwa na uchakavu mkubwa wa majengo ya madarasa, hali inayohatarisha mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji, hususan wakati wa mvua na upepo mkali.

Alisema shule hizo zinakabiliwa na uhaba wa vyoo vya kisasa, jambo linalochangia changamoto za usafi na afya kwa wanafunzi na walimu, huku akisisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu.

Mbali na sekta ya elimu, Mrutu alisema wananchi wa Shighatini wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa zahanati katika kijiji cha Shighatini, hali inayowalazimu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Pia alitaja changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na hali mbaya ya baadhi ya barabara zinazounganisha vijiji na maeneo ya uzalishaji, akisema changamoto hizo zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wao, baadhi ya Wenyekiti wa viijiji vya Lambo Majid Swed Temba na Mwenyekiti wa kijiji cha Vuchamandabwe Swafia Lusomya walisema vyoo vya Shule za Msingi Momba na Vuchamandabwe vipo katika hatari ya kuzama kutokana na hali ya mazingira ya maeneo hayo, na kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka ili kuondoa hatari inayoweza kuhatarisha afya na usalama wa wanafunzi.

Akijibu changamoto zilizowasilishwa na wananchi wa kata ya Shinghatini Mbunge wa Mwanga Dk. Ngwaru Maghembe, alisema tangu achaguliwe kuwa Mbunge wa jimbo hilo, zaidi ya vijana 70 ameweza kuwatafutia kazi sehemu mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu na kwenye majeshi ya ulinzi na usalama.

Aidha alisema amezipokea changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi ikiwemo ile ya miundombinu ya shule, uhaba wa vyoo, changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, sanjari na ubovu wa barabara na kuahidi kuzifanyia kazi.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.