MOSHI-KILIMANJARO.
MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Shadrack Mhagama, amesema kuwa kuundwa kwa Kamati Maalum ya Serikali ya Tanzania ya kusimamia urejeshaji wa mabaki ya machifu wa zamani pamoja na mali kale zilizochukuliwa wakati wa ukoloni, kutakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa na kuhifadhi historia ya nchi kwa vizazi vijavyo.
Mhagama alitoa kauli hiyo Juni mosi, 2026 wakati wa mkutano wa wadau wa maendeleo uliofanyika mjini Moshi kwa lengo la kujadili na kushauriana kuhusu uanzishwaji wa makumbusho ya mkoa, ambayo itakuwa jengo la zamani lililokuwa likitumiwa na Mangi wa Wachaga lililopo eneo la KDC.
Mhagama alisema mwaka 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliunda kamati maalum ya kusimamia mchakato wa kurejesha mabaki ya machifu na mali za kihistoria zilizochukuliwa wakati wa ukoloni, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, wakati wa ziara yake jijini Dar es Salaam.
“Urejeshaji wa mabaki hayo unalenga kurejesha maelfu ya vitu vya kitamaduni na kihistoria vilivyochukuliwa wakati wa ukoloni. Vitu hivyo vikirejeshwa vitasaidia kuhifadhi historia ya taifa kupitia makumbusho tunayotarajia kuanzisha hapa Moshi,” alisema Mhagama.
Aliongeza kuwa mali na mabaki mengi ya kihistoria kutoka Tanzania yalipelekwa katika nchi mbalimbali ikiwemo Ujerumani, Hungaria na mataifa mengine ya Ulaya, huku suala la kurejeshwa kwa kichwa cha Chifu wa Old Moshi, Mangi Meli, likiwa miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele
.
Akiwasilisha mada kuhusu makumbusho ya MDC, Mratibu wa Makumbusho hayo, Dk. Venance Silayo, alisema kuna zaidi ya mabaki 100,000 yanayohusiana na Watanzania yaliyohifadhiwa nchini Ujerumani, zaidi ya 2,000 nchini Hungaria, pamoja na mengine mengi yaliyoko katika nchi kama Uingereza na Ufaransa.
Dk. Silayo alisema jambo la kutia matumaini ni kuwa taasisi nyingi zinazohifadhi mabaki hayo zimeonyesha utayari wa kushirikiana katika mchakato wa kuyarejesha Tanzania, hatua itakayorahisisha utekelezaji wa azma ya Serikali ya kurejesha urithi wa taifa.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa MDC, Beno Chuwa, alisema maendeleo ya sayansi ya vinasaba yamekuwa na mchango mkubwa katika kutambua mabaki ya watu waliokuwa wamehifadhiwa katika makumbusho ya Ulaya.
Alisema kupitia uchunguzi wa vinasaba, watafiti wamefanikiwa kubaini mafuvu ya baadhi ya viongozi wa jadi wa Tanzania, akiwemo Chifu Lobulu Kaaya wa Arumeru mkoani Arusha pamoja na Chifu Molelia na Chifu Mkunde wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa ya Tanzania, Dk. Noel Lwoga, Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini wa Makumbusho ya Taifa, Agnes Robert, aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kwa kuanzisha wazo la kujenga makumbusho hayo.
Alisema makumbusho hayo yatakuwa sehemu muhimu ya kuhifadhi historia, utamaduni na urithi wa Watanzania, huku yakifungua fursa za utalii wa kihistoria na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Katika mkutano huo, washiriki pia walipata fursa ya kujifunza matokeo ya utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti na Habari cha Marejesho kuhusu mchakato wa urejeshaji wa mabaki ya mababu na mali za kitamaduni katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Mratibu wa mpango huo kutoka nchini Ujerumani, Kondradini Kwazo, alisema utafiti huo unalenga kuunganisha mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na taasisi zinazohifadhi mabaki ya mababu pamoja na mali za kitamaduni zilizopo nchini Ujerumani, huku matokeo yake yakitarajiwa kuwa msingi muhimu katika uanzishwaji wa makumbusho ya mkoa wa Kilimanjaro.
![]() |















